Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MAJOHE WAONGEZEWA KILOMITA 81 ZA MTANDAO WA MAJI
29 Jun, 2026
MAJOHE WAONGEZEWA KILOMITA 81 ZA MTANDAO WA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuongeza mtandao wa huduma ya maji katika Kata ya Majohe, Wilaya ya Ilala, hatua itakayowezesha zaidi ya wakazi 1,600 kupata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.

Mradi huo ambao umelenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji na kukidhi mahitaji ya wananchi wa Kata ya Majohe, unahusisha kazi za ulazaji wa mabomba yenye kipenyo cha inchi 8, 6, 3 na 2 kwa urefu wa kilomita 81 pamoja na kuwaunganisha huduma wakazi wa eneo hilo.

Maeneo yatakayonufaika na mradi huu wa maji ni Mitaa ya Majohe Four by Four, Majohe Halisi, Majohe Rada, Majohe Kichangani, Kwa Mkandawile, Chadema Pamoja, Kwa Warioba, Mikanjuni na Viwege.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Msimamizi wa Mradi, Mhandisi Ramadhani Sangali  amesema kazi za ulazaji wa mabomba na uunganishaji wa wateja zinaendelea kwa kasi ili wananchi waanze kupata huduma mapema kadri maeneo yanavyokamilika.

"Kwa sasa tunaendelea na kazi katika mitaa ya Four by Four na Kwa Warioba, sambamba na hilo tunaunganisha wateja katika maeneo ambayo tayari yamefikiwa na mabomba bila kusubiri mradi mzima ukamilike, ili wananchi waanze kunufaika mapema," amesema Mhandisi Sangali.

Mkazi wa Mtaa wa Majohe Halisi, Tumaini Kilima, amesema ujio wa huduma hiyo utapunguza gharama za kununua maji na kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwawezesha kupata maji safi na salama kwa urahisi.

"Tunafurahia kuona mabomba yamefika mtaani kwetu. Hii ni hatua kubwa ambayo itarahisisha upatikanaji wa maji na kupunguza gharama tulizokuwa tunatumia kununua maji. Tunaishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kutuletea huduma hii muhimu," amesema.

Mradi wa Majohe ni sehemu ya juhudi za DAWASA za kuendelea kupanua mtandao wa huduma ya maji katika maeneo mbalimbali ya Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya Majisafi salama na ya uhakika.