Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAWAFUATA WANANCHI WILAYA YA UBUNGO
07 Feb, 2026
DAWASA YAWAFUATA WANANCHI WILAYA YA UBUNGO

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imefungua dawati la huduma kwa wateja katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto za huduma ya maji zinazowakabili wananchi, hususan wa Jimbo la Kibamba.

Akizungumza katika dawati hilo, Afisa Huduma kwa Wateja wa DAWASA, Ndugu Juliana Simon amesema hatua hiyo inalenga kusogeza huduma karibu na wananchi ili kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama na ukusanyaji wa maoni kuhusu huduma zetu.

“Kupitia dawati hili, tunapokea kero za wananchi moja kwa moja, tunazifanyia kazi kwa haraka na kuzifuatilia hadi zipate ufumbuzi. Lengo letu ni kuhakikisha changamoto za maji Kibamba zinatatuliwa kwa wakati,” amesema Ndugu Juliana.

Wananchi wamejitokeza kupata huduma, wamepongeza hatua hiyo, wakieleza imeleta nafuu na kupunguza usumbufu wa kufuata huduma katika ofisi za mbali.

Mmoja wa wananchi wa Jimbo la Kibamba, Ndugu Benedict Siwi amesema uwepo wa DAWASA leo katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Ubungo umeongeza matumaini ya kutatuliwa kwa changamoto za muda mrefu za maji.

“Awali tulikuwa tunapata ugumu mkubwa kufuata huduma za DAWASA, lakini leo nimepata urahisi kwa kufikisha malalamiko yangu na kupata majibu hapahapa. Naamini changamoto zetu zitapatiwa ufumbuzi,” amesema Siwi.

DAWASA inaahidi kuendelea kuboresha huduma zake kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na wananchi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa uhakika katika Jimbo la Kibamba na maeneo jirani.