Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAWAHIMIZA WATEJA MAGOMENI KUKAMILISHA MALIPO YA HUDUMA ZA MAJI
25 Mar, 2025
DAWASA YAWAHIMIZA WATEJA MAGOMENI KUKAMILISHA MALIPO YA HUDUMA ZA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkoa wa kihuduma Magomeni imewahimiza Wakazi na Wananchi wanaohudumiwa na Mamlaka kulipa bili za mwezi kwa wakati ili kuwezesha Mamlaka kuboresha zaidi huduma zake.

Afisa Biashara DAWASA Magomeni, Ndugu Prisca Makenya amesema kuwa kupitia Mkataba wa huduma kwa wateja umeainisha kuwa mteja anao wajibu wa kulipia ankara yake ya Maji kwa wakati kulingana na matumizi yake ya mwezi husika.

"DAWASA imeweka dhamira ya kufikisha huduma kwa wateja wote kwa ubora. Hivyo ni vyema wananchi wakafahamu kuwa Mamlaka inategemea makusanyo ili kutekeleza miradi ya usambazaji maji pamoja na kuendelea kuwahudumia wananchi" amesema.

Ndugu Makenya amesema kuwa zoezi la ufuatiliaji wateja wenye madeni nyumba kwa nyumba linaendelea katika maeneo mbalimbali ndani ya eneo letu la kihuduma.

"Tunawasisitiza wateja wote wawe na utamaduni wa kulipa bili zao bila kulaza deni ili waweze kumaliza mwezi huu bila deni lolote la maji kutoka kwetu," ameeleza.

Mkoa wa kihuduma DAWASA - Magomeni unahudumia wateja takribani 25,190 katika kata 11 za Tandale, Sinza, Manzese, Mabibo, Kigogo, Magomeni, Makurumla, Ubungo, Mburahati, Mzimuni na Ndugumbi.