DAWASA YAWAPA 'SUBRA' YA MUDA WAKAZI MSEWE NA GOLANI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa suluhu ya muda mfupi ya changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wakazi wa Golani na Msewe kwa kusogeza huduma ya maji kupitia maboza ili kuondoa makali ya ukosefu wa maji.
Hatua hiyo imekuja baada ya maeneo hayo kuwa ni miongoni mwa maeneo yanayopata huduma ya maji kwa mgao na ratiba yao ya Maji kuathiriwa na matengenezo ya Mtambo wa Ruvu Juu yaliyofanyika mapema wiki hii.
Akizungumzia zoezi hilo, Meneja wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma Ubungo, Mhandisi Damson Mponjoli amesema zoezi hili limefanyika kutokana na eneo la Golani kuathirika na changamoto ya ukame na huduma iliporejea pakatokea changamoto ya uvujaji katika bomba la inchi 6 linalosambaza maji katika eneo hilo.
"Golani ni eneo mojawapo lililoathirika kutokana na hitilafu Mtamboni, lakini baada ya huduma ya maji kurejea, kukatokea hitilafu ya kupasuka kwa bomba la inchi 6 na kuongeza changamoto kwa wananchi, lakini tumeamua kama Mamlaka kutumia njia ya muda mfupi ya kuleta maji kwa maboza bila malipo ili waendelee kupata maji tukiendelea na uimarishaji wa huduma.," amesema Mhandisi Mponjoli.
Maria Nelson Mshani, Mkazi wa Msewe ameishukuru DAWASA kwa kuchukua hatua ya kuleta maji kupitia maboza na itasaidia kupunguza changamoto za kihuduma na kijamii.
