Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAWASHIKA MKONO MAKUNDI MAALUM SEKONDARI YA PUGU
12 Mar, 2026
DAWASA YAWASHIKA MKONO MAKUNDI MAALUM SEKONDARI YA PUGU

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imetoa msaada kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Sekondari Pugu, wilayani Ilala.

Msaada huo ni sehemu ya mchango wake kwa jamii na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha ustawi wa jamii inayoihudumia.

Aidha, msaada huo umegharimu zaidi ya Shilingi Milioni 3 na umehusisha kulipa gharama za bima za afya kwa wanafunzi zaidi ya 30, viti mwendo na taulo za watu wazima (Adult diapers) kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA, Ndugu Everlasting Lyaro amesema Mamlaka inaendelea kutambua umuhimu wa kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili hususan makundi yenye uhitaji maalum na ndio maana Mamlaka inaendelea kutoa misaada mara kwa mara.

“DAWASA tunaamini maendeleo ya jamii msingi wake ni afya bora na ndio maana tumeleta bima za afya, tumewekeza kwenye afya za vijana wetu ili kuwajengea uhakika wa kupata uangalizi wa kiafya na kuendelea na masomo bila vikwazo.

Pugu ni nyumbani, tumekuwa tukija mara kwa mara na tunaamini kupitia msaada huu wanafunzi watapata mazingira bora ya kujifunzia na kuishi wakiwa shuleni," amesema Ndugu Lyaro.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu, Ndugu Patrick Sinyinza ameishukuru DAWASA kwa msaada huo, akieleza utasaidia kuboresha ustawi wa wanafunzi wenye mahitaji maalum na kuwapa fursa bora zaidi ya kuendelea na masomo yao bila vikwazo vinavyotokana na changamoto za kiafya.

"Tunawashukuru sana kwa kujali afya za wanafunzi wetu kwani ndio mtaji pekee walionao, msaada huu utakwenda kuongeza hamasa ya masomo kwao kwani umefikia yale mahitaji maalum, nitoe rai kwa wanafunzi njia pekee ya kulipa fadhila kwa wadau hawa ni kuendelea kuongeza bidii na kuonyesha ulemavu sio kikwazo cha kupata elimu bora," amesema Mwalimu Sinyinza

Naye, Mwanafunzi wa kidato cha nne, Ndugu Thobias Masumbuko akitoa neno la shukrani ameishukuru DAWASA kwa kuona umuhimu wa kuwasaidia kwani wengi wao wametoka katika familia zenye kipato cha chini na mda mwingine hawana fedha kwa ajili ya matibabu lakini DAWASA wamewawezesha kupata bima za afya ambazo zitawasaidia kupata matibabu bila shida yoyote.

DAWASA imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za uwajibikaji kwa jamii (CSR) zikiwemo kusaidia sekta ya afya, elimu pamoja na utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu huduma za majisafi na usafi wa mazingira ili kuhakikisha huduma zinapatikana kwa ufanisi zaidi.