Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAWEKA KAMBI MAKONGO KUTATUA CHANGAMOTO ZA HUDUMA YA MAJI
20 Feb, 2026
DAWASA YAWEKA KAMBI MAKONGO KUTATUA CHANGAMOTO ZA HUDUMA YA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkoa wa Kihuduma Makongo wametembelea mitaa ya eneo la Makongo yenye changamoto ya upatikanaji wa maji kwa muda mrefu kwa lengo la kubaini tatizo na kuainisha mipango ya muda mrefu na mfupi iliyopo ya kutatua changamoto hizo. 

Akizungumza wakati wa zoezi hilo katika Mtaa wa Kimara Baruti,  Afisa Huduma kwa Wateja DAWASA, Ndugu Christopher Sika amesema maeneo ya kwa Nguya, Ngowi Mkwavi, Maduka Sita, Msikitini na Nguzo 770 yamekuwa yakipata huduma ya maji kwa msukumo mdogo na baadhi ya wateja wamekuwa wakikosa maji kwa kipindi kirefu lakini Mamlaka imejipanga kikamilifu kutatua changamoto hiyo.

"Katika maeneo haya kila wiki kuanzia sasa tutahakikisha yanapata huduma ya maji mara mbili kwa siku, yani Alhamisi na Ijumaa, na tutaelekeza maji katika eneo hili, lakini kwanza tunakwenda kuanza kazi ya kuongeza msukumo wa maji kutoka bomba la inchi 8 kwenda inchi 4 ili kuhakikisha changamoto hii inakwisha," amesema Ndugu Sika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa wa Kimara Baruti, Ndugu Rick Mbusi amesema wamepitia changamoto ya maji kwa kipindi cha takribani miezi miwili hadi mitatu, anawashukuru DAWASA kwa kuwa wasikivu kwa kufika eneo hilo kutatua changamoto hiyo. 

"DAWASA wametueleza mipango yao ya kumaliza changamoto hii, nisisitize kwenye usimamizi wa ratiba waliyotupatia tuweze kupata maji siku ya Alhamisi na Ijumaa kila wiki kikamilifu, huku wakiwa wanaendelea na mpango wa kuongeza msukumo wa maji katika mtaa wetu, tutaendelea kufatilia na kufanya nao kazi kwa karibu kuhakikisha kazi mpango huu unatekelezeka," amesema Ndugu Mbusi.

Mbusi amewaomba wananchi wa eneo lake kuendelea kuwa watulivu kwa kipindi hiki cha mpito kwani wana imani na DAWASA katika kutatua changamoto hii mapema.