Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAWEKA MIKAKATI YA KUONGEZA UFANISI KWA WATENDAJI
09 Sep, 2026
DAWASA YAWEKA MIKAKATI YA KUONGEZA UFANISI KWA WATENDAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza kutekeleza mfumo wa upimaji wa utendaji kazi (Key Perfomance Indicator) kwa watendaji wake kupitia utiaji saini wa makubaliano ya utendaji kazi kwa Mwaka wa fedha 2026/2027, hatua inayolenga kuongeza uwajibikaji, ufanisi na utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia matokeo.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo na Mameneja wa Mikoa kazi ya DAWASA, ambapo kila mtendaji amewekewa viashiria na malengo ya utendaji yatakayopimwa katika kipindi cha mwaka mmoja.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangingo, amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuhakikisha kila mtendaji anawajibika katika eneo lake na taasisi inafikia malengo yaliyowekwa.

“Tunapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia viashiria tulivyokubaliana. Kila mmoja awajibike katika eneo lake na tushirikiane kuhakikisha tunapata ufanisi na matokeo yanayotarajiwa,” amesema Mhandisi Mwangingo.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amesema makubaliano hayo yanaainisha wajibu wa mtumishi na mwajiri katika upimaji wa utendaji, hivyo wasimamizi wanapaswa kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanatekelezwa na kutathminiwa kwa wakati.

Amesema malengo ya mwaka wa fedha 2026/2027 yametokana na Mpango wa Biashara wa DAWASA wa miaka mitano na ni sehemu ya utekelezaji wa mwelekeo wa kimkakati wa Mamlaka.

Mhandisi Bwire ameongeza kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo utafanyiwa tathmini za mara kwa mara ili kufuatilia maendeleo, kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kuhakikisha malengo yanafikiwa kwa ufanisi, hatua inayolenga kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.