Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAZIDI KUTEKELEZA AGIZO LA KUBORESHA HUDUMA KUPITIA VISIMA KISUKURU
12 May, 2026
DAWASA YAZIDI KUTEKELEZA AGIZO LA KUBORESHA HUDUMA KUPITIA VISIMA KISUKURU

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) imekamilisha zoezi la upimaji wa wingi wa maji katika kisima kipya cha Kisukuru eneo la Viwanja vya Benki ambapo kimethibitika kuwa na uwezo wa kuzalisha takribani Lita 144,000 kwa siku.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Msimamizi wa mradi Mhandisi Phylemon Ojode amesema upimaji wa kisima hicho umeonesha kisima kina uwezo wa kuzalisha lita 6,000 kwa saa ambazo ni sawa na lita 144,000 za maji kwa siku zitakazotumika kuimarisha nguvu katika maeneo ya Kisukuru, Mianzini na Kihimbwa kwa matumizi ya wananchi pamoja na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi. 

"Tumekamilisha zoezi la majaribio ya pampu ambalo kitaalam ni mahususi kwa ajili ya kupima uwezo wa uzalishaji wa kisima hiki ambacho kwa sasa tumefahamu kina uwezo wa kuzalisha Lita 144,000, zitakazotumika kuimarisha Usambazaji wa Maji kwa wakazi wa Kisukuru, Mianzini na Kihimbwa," amesema Mhandisi Ojode. 

Aidha, Mhandisi Ojode ameeleza kuwa kwa sasa hatua inayoendelea ni kupima ubora wa maji ambapo DAWASA inafanya vipimo zaidi vyenye lengo la  kuhakikisha maji hayo yanakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Mwenyekiti wa Mtaa Kisukuru, Ndugu John Masele ametoa rai kwa DAWASA kuhakikisha inakamilisha taratibu zote kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na kisima hicho ambacho kitarahisisha utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
 
Mradi wa uchimbaji kisima hicho ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma ya maji katika maeneo mbalimbali ndani ya eneo la kihuduma la DAWASA, ambapo Serikali imeendelea kuwekeza katika miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika.