Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
"SEKTA BINAFSI ITUMIKE KUIMARISHA HUDUMA YA MAJI" - MHANDISI KUNDO
12 May, 2026
"SEKTA BINAFSI ITUMIKE KUIMARISHA HUDUMA YA MAJI" - MHANDISI KUNDO

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Mathew Kundo amesisitiza juu ya umuhimu wa Wizara ya Maji kushirikiana na Sekta binafsi nchini kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kufanikisha malengo ya Serikali ya utoaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi wote kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2030. 

Hayo ameyasema wakati wa ufunguzi wa kongamano lililoandaliwa na Kituo cha Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC)lenye lengo la kujadili nafasi ya ubia katika maendeleo ya Sekta ya maji nchini. 

Kongamano hilo limeshirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo katika kujadili hali ya uboreshaji wa huduma ya maji ambapo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)ilikuwa mojawapo ya washiriki katika kongamano hilo. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo Mhandisi Kundo amesema ushiriki wa Sekta Binafsi ni muhimu katika kufanikisha malengo ya Wizara ya Maji ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma endelevu ya majisafi na salama.

"Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tayari imeandaa Mkakati wa Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi (Private Sector Investment Strategy) utakaowezesha kuongeza uwekezaji, ubunifu na ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maji nchini," amesema Mhandisi Kundo. 

Ameongeza kuwa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi utaongeza uwezo wa kifedha na kitaalamu katika kuimarisha huduma kwa wananchi na utasaidia kutekelezwa kwa Dira ya 2050 ambayo inaelekeza kuitumia Sekta Binafsi kama mhimili wa kuendesha uchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi na Uwekezaji, Mhandisi Ramadhan Mtindasi amesema tayari DAWASA imefanya Ubia na Sekta binafsi haswa katika kudhibiti upotevu wa maji, ambapo juhudi hizo zimesaidia kupunguza kiwango cha upotevu wa maji Katika Kanda ya Kinondoni.

"Ni ukweli usiopingika kuwa tunakaribisha wawekezaji katika juhudi zetu za kusambaza Maji pamoja na kudhibiti upotevu wa Maji, tayari tumeshaanza Kwa Kinondoni na sasa tunawakaribisha wawekezaji kwani tayari tunayo miradi ya kimkakati inayohitaji uwekezaji ikiwemo Mradi wa maji Rufiji," amesema Mhandisi Mtindasi.

Kupitia ushiriki wake katika kongamano hilo, DAWASA imeendelea kuonesha dhamira yake ya kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutafuta suluhisho endelevu na bunifu kwa ajili ya kuboresha huduma za maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani.