DAWATI LA DAWASA OFISI YA MKUU WA MKOA LAVUTIA WANANCHI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea na dawati la huduma kwa wateja katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kusogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha changamoto zinazohusu huduma za maji na usafi wa mazingira zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Dawati la Huduma kwa wateja linalenga kushughulikia changamoto na kupokea mrejesho wa huduma, kutoa elimu kuhusu huduma za majisafi na usafi wa mazingira, elimu ya udhibiti wa upotevu wa maji pamoja na kuwapatia wateja taarifa sahihi kuhusu miradi na maboresho yanayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa wateja, Ndugu Haruna Taratibu amesema uwepo wa dawati la huduma kwa wateja ni moja ya ya mkakati wa Mamlaka katika kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa kuwafikia katika maeneo yao badala ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika ofisi za DAWASA.
“Mamlaka inaendelea kuboresha huduma kwa wateja wetu kwa kuwafuata wananchi walipo ili kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa haraka. Dawati hili litasaidia sana kuimarisha mawasiliano kati ya Mamlaka na wananchi na na kupelekea kuboresha utoaji wa huduma,” amesema Ndugu Taratibu
Wananchi waliotembelea madawati hayo wamepongeza hatua hiyo wakieleza kuwa imewapa fursa ya kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja na kupata majibu kwa wakati, jambo linaloongeza ufanisi wa huduma kwa wateja.
Ndugu Sudi Mpili Mkazi wa Bonyokwa amepongeza Mamlaka kwa kuleta huduma karibu jambo ambalo linaongeza ufanisi wa huduma kwa wateja.
"Niwapongeze DAWASA kwa hatua hii kwa upande wangu nilikua nashughuli nyingine katika ofisi hizi lakini nimepata nafasi ya kuhudumiwa changamoto yangu ya maji, zoezi hili liwe endelevu na mfike na mitaani pia ili mfikie wananchi wengi zaidi" amesema Ndugu Mpili
Mamlaka inaendelea na kufungua madawati ya huduma kwa wateja katika ofisi zote za Wilaya za Mkoa wa Dar es salaam na Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, kwa wakati na zenye kuzingatia ubora.
