EWURA YATEMBELEA KIDUNDA, YASHAURI KASI YA UKAMILISHAJI
Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji Nchini (EWURA) imeipongeza Serikali kwa utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa kihistoria wa Bwawa la Kidunda utakaosaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.
Mwenyekiti wa Bodi EWURA, Profesa Mark Mwandosya ameyasema hayo wakati wa ziara ya Bodi kutembelea na kujionea hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi zinazoendelea.
Ameeleza kuwa Bwawa la Kidunda ni mradi mkubwa wa kimkakati ambao kwa muda mrefu Serikali imekuwa na nia ya dhati ya kutekeleza kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma ya majisafi katika Mikoa ya Dar na Pwani hususani kipindi cha upungufu wa Maji.
"Tumetembelea na tumejionea namna mradi ulivyotekelezwa kwa kuzingatia ubora, viwango na thamani ya fedha imeonekana na hivyo kuridhika kiwa utekelezaji wake unaenda vizuri mpaka sasa na utakuwa muarobaini wa Changamoto ya huduma pindi utakapokamilika" amesema Profesa Mwandosya.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DAWASA, Mhandisi Elizabeth Kingu amesema utekelezaji wa mradi wa Maji Kidunda umefikia asilimia 40 na unategemea kukamilika Desemba 2026 na utekelezaji wake utagharimu takribani Bilion 337 hadi kukamilika kwake.
