EWURA YAWAPA NONDO DAWASA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dkt. James Mwainyekule amesisitiza umuhimu wa maofisa huduma kwa wateja kuwa wabunifu katika kuhudumia wateja na kutochukulia kazi kwa mazoea.
Amesema hatua hiyo itapunguza malalamiko yanayotolewa mara kwa mara na wateja bila kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Dkt. Mwainyekule ameyasema hayo leo Alhamisi, Juni 26, 2025 wakati akifugua semina ya siku moja iliyolenga kutathmini hali ya huduma kwa wateja na kuwashirikisha maofisa huduma kwa wateja kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA).
"Ustawi wa wananchi unategemea huduma hizi tunazozitoa kwao, niwaombe kuwa wabunifu na kutochukulia kazi kwa mazoea ili kila siku tuweze kuboresha utoaji huduma kwa wateja na wananchi waone matunda ya uwekezaji unaofanywa na Serikali yao katika kuwafikishia huduma ya maji," amesema Dkt. Mwainyekule.
Amesema EWURA ipo tayari kushirikiana na DAWASA katika maeneo yanayolenga kuboresha utoaji huduma kwa wateja na kusisitiza baada ya semina hiyo kwa pamoja waje na mawazo bora ya kuimarisha huduma kwa wateja katika Jiji la Dar Es Salaam na mkoa wa Pwani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja (DAWASA) CPA (T), Rithamary Lwabulinda amesema taasisi wanashukuru kupatiwa nafasi hiyo ya mafunzo kwani lengo ni kutoa huduma bora kwa wateja wote.
"Tunaishukuru EWURA kwa kutupatia nafasi hii kuendelea kuelimishana, kwani hata sisi DAWASA lengo letu ni kutoa huduma bora kwa wateja wetu wote, hapa tunapata fursa ya kuelezwa baadhi ya mambo ambayo sisi hatuyasikii moja kwa moja toka wateja lakini EWURA kama mdhibiti na msimamizi wetu anayapata," amesema Rithamary.