Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
HUDUMA YA MAJI YAREJEA KIBONDE MAJI BAADA YA MATENGENEZO
27 Oct, 2026
HUDUMA YA MAJI YAREJEA KIBONDE MAJI BAADA YA MATENGENEZO

Huduma ya maji imeanza kurejea kwa wakazi wa Kibonde Maji, Kata ya Mbagala, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kufanya maboresho ya bomba lenye kipenyo cha inchi sita lililoathiri usambazaji wa maji katika eneo hilo.

Maboresho hayo yamefanywa na DAWASA Mbagala ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu na kuongeza ufanisi wa usambazaji wa majisafi kwa wananchi.

Akizungumzia hatua hiyo Mhandisi Richard Kaloli, amesema maboresho hayo yanalenga kuimarisha miundombinu na kupunguza changamoto zinazoweza kuathiri upatikanaji wa huduma ya maji.

“Tunafanya maboresho haya ili kuimarisha mabomba na kuwezesha usambazaji wa maji kwa ufanisi zaidi kwa wananchi. DAWASA itaendelea kufuatilia hali ya miundombinu yake ili kubaini na kutatua changamoto zinazoweza kuathiri upatikanaji wa huduma ya maji,” amesema Kaloli.

Kwa upande wake, mkazi wa Kibonde Maji, Abdukadil Shamte, ameishukuru DAWASA kwa hatua hiyo, akisema kurejea kwa huduma kumewapunguzia usumbufu wa kutafuta maji kwa umbali mrefu.

“Tunaishukuru DAWASA kwa juhudi za kurejesha huduma ya maji, kwani hatua hiyo imetupa nafuu ya kutafuta maji kwa umbali mrefu, ikizingatiwa kuwa maji ni hitaji muhimu katika shughuli za kila siku,” amesema Shamte.