HUDUMA YA MAJI YAWAFIKIA VISIGA, WANANCHI WAPONGEZA
Takribani wakazi 800 wa Kata ya Visiga, mtaa wa Visiga Kati na Saini wameanza kupata huduma ya majisafi baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kutekeleza mradi wa maji maeneo hayo ambao umefikia zaidi ya asilimia 85.
Mradi huo umehusisha ujenzi wa mtandao wa mabomba ya maji ya inchi 4,3 na 2 kwa umbali wa kilomita 5, na unanufaisha wakazi wa maeneo hayo na kusaidia upatikanaji mzuri wa huduma ya majisafi.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wake, Msimamizi wa mradi kutoka DAWASA Mlandizi, Mhandisi Ally Migeyo amesema kazi inaendelea vizuri na hatua kubwa tayari imefikiwa kwa kuwa maeneo ambayo tayari wamekamilisha kuweka miundombinu wananchi wanaendelea kupata huduma ya majisafi.
"Mradi wa maji Visiga umefikia asilimia 90 ya utekelezaji na tayari baadhi ya wateja wameanza kupata huduma ya maji. Kazi zilizobaki ni chache na tunaendelea kuzitekeleza kwa kasi ili kila wananchi wa eneo hili wapate huduma ya majisafi,” amesema Migeyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Visiga Kati, Ndugu Said Kupika, ameipongeza DAWASA Mlandizi kwa kusimamia vyema utekelezaji wa mradi huo, akibainisha umepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya maji katika mtaa huo.
"Mradi huu umeleta mabadiliko makubwa kwa wananchi wa Visiga Kati. Upatikanaji wa maji umeimarika na maisha ya wakazi wetu yanaendelea kuboreka,” amesema Kupika.
Ndugu Agness Haule, mkazi wa mtaa wa Visiga, ameeleza kuridhishwa na hatua ya mradi huo kwani huduma ya maji imeanza kuleta faraja kwa familia nyingi, na kuomba Mamlaka izidi kufikia zaidi kwenye maeneo mengine ambayo hayana huduma.
“Kwa muda mrefu tulikuwa tukipata shida ya maji, lakini sasa maji yameanza kufika majumbani. Tunashukuru sana DAWASA kwa kutekeleza mradi huu, tuna imani na DAWASA sasa kwamba wanatusikiliza na kutekeleza kwa wakati," amesema Ndugu Agness.
