KAMATI YA BUNGE YAPONGEZA UTEKELEZAJI MRADI BWAWA LA KIDUNDA
Kamati ya Bunge ya Maji na Mazingira imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha Shilingi Bilioni 335 ili kutekeleza mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda, mkoani Morogoro.
Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Jackson Kiswaga (Mb) imebainisha hayo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wa mkakati wa Bwawa la Kidunda.
"Tunajivunia mradi huu ambao tumetekeleza kwa fedha za Watanzania wenyewe, ni mradi muhimu sana kwani utaleta utulivu wa huduma ya maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani hususani kipindi cha ukame na mabadiliko ya tabianchi," amesema Mheshimiwa Kiswaga.
Mheshimiwa Kiswaga amesema Kamati ya Bunge Maji na Mazingira itahakikisha inaishauri Serikali vizuri ili fedha za utekelezaji wa mradi huu zisikwame na mradi ukamilike kwa wakati na manufaa yake yaonekane.
"Tutafanya jukumu letu kuishauri Serikali mradi uwezeshwe ili kukamilika kwa wakati, lakini niwaombe wananchi watunze vyanzo vya maji kwani ndio uhai wa Bwawa hili litakapokamilika, uchafuzi wa vyanzo utapelekea ujaaji wa tope katika Bwawa na kupunguza miaka ya Bwawa iliyopangwa kufanya kazi hivyo kuleta hasara," amesema Mheshimiwa Kiswaga.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Ndugu Rose Ambrose amesema Wizara ya Maji itaendelea kusimamia vyema utekelezaji wa mradi huu na kuhakikisha inatatua vikwazo vyote ili mradi ukamilike kwa wakati na kuleta tija kwa wananchi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire amesema mradi wa Bwawa la Kidunda umefikia asilimia 47 ya utekelezaji wake huku mategemeo yakiwa kukamilisha mradi ifikapo Disemba 2026.
Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda utahusisha Bwawa lenye uwezo wa kuhifadhi maji Lita bilioni 19 0, uzalishaji umeme megawati 20, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe kilomita 75 toka Ngerengere hadi Kijiji Cha Kidunda.
