Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
KAMATI YA BUNGE YAVUTIWA NA UWEKEZAJI MIRADI YA DAWASA
27 Mar, 2026
KAMATI YA BUNGE YAVUTIWA NA UWEKEZAJI MIRADI YA DAWASA

Kamati ya Kudumu ya Bunge Uwekezaji na Mitaji ya Umma imeipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)kwa jitihada kubwa za kutekeleza miradi mikubwa ya majisafi na ya kuboresha Usafi wa Mazingira yenye kuleta tija ya upatikanaji wa huduma kwa wananchi sambamba na kuthaminisha uwekezaji unaofanywa na Serikali. 

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge Mhe. Masanja Kadogosa (Mb)mara baada ya kutembelea utekelezaji na uboreshaji wa miradi ya majisafi ikiwemo Mtambo wa kuzalisha maji Ruvu Chini pamoja na mradi wa kuboresha usafi wa mazingira wa Mbezi Beach unaotekelezwa na Mamlaka. 

Amesema kuwa Kamati imetembelea na kuona thamani ya uwekezaji mkubwa uliofanywa katika Mtambo wa kuzalisha maji wa Ruvu Chini pamoja na maboresho yanayotekelezwa yanayolenga kuongeza na kuimarisha upatikanaji mzuri wa huduma ya majisafi. 

"Pia, kamati imetembelea utekelezaji wa mradi wa uboreshaji huduma za usafi wa mazingira katika eneo la Mbezi Beach unaolenga kunufaisha wananchi wa Mbezi beach, Salasala, Mbezi juu na maeneo ya jirani, kazi imefikia hatua nzuri," ameeleza Mhe. Kadogosa. 

"Tuipongeze sana DAWASA kwa kazi kubwa waliyoitekeleza, sambamba na mipango madhubuti waliyojiwekea ya kuboresha huduma ambayo wanaitekeleza kikamilifu ikiwemo mradi wa Bwawa la Kidunda, mradi wa Rufiji na mradi wa Visima vya kuongeza uzalishaji wa maji, vyote hivi kwa ujumla vinasaidia kuleta unafuu katika upatikanaji wa huduma ya majisafi, " amesema Mhe. Kadogosa. 

Ameitaka DAWASA kuwa na utaratibu wa kufanya maboresho ya mara kwa mara ya miundombinu ya maji ili iweze kudumu kwa muda mrefu na iendelee kutoa huduma kwa wananchi. 

Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali kupitia DAWASA kuwa waaminifu katika utunzaji wa miundombinu ya majisafi na Usafi wa Mazingira ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kutoa huduma ya uhakika kwa kipindi chote. 

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa kwa sasa eneo ambalo Mamlaka inahudumia lina jumla ya wakazi milioni 7,400,000 na mahitaji ya maji kwa siku ni lita milioni 772 kwa siku. Kwa sasa uwezo wa uzalishaji wa maji ni lita milioni 553 kwa siku na hivyo kuna upungufu wa huduma kwa lita milioni 219. 

"Hata hivyo, Mamlaka imejipanga kwa kina kuhakikisha inaboresha na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa maji kwa kupanua mtambo wa Ruvu Chini kwa kuongeza uwezo wa lita milioni 90 za maji kwa siku ili kufikia uwezo wa lita milioni 360 za maji kwa siku," ameeleza. 

"Pia tunalenga kuboresha na kuongeza upatikanaji wa huduma kupitia utekelezaji wa mradi wa mkubwa wa Bwawa la Kidunda linalojengwa Morogoro, pamoja na Mtambo wa Kuzalisha maji wa Rufiji unaotarajiwa kujengwa katika eneo la Rufiji utakaosadia kwa kiasi kikubwa kutoa huduma kwa wananchi wa Rufiji, Mkuranga, Kisarawe na Dar es Salaam," amesema Mhandisi Bwire. 

Ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mamlaka katika kuwezesha utekelezaji wa miradi ya majisafi na usafi wa mazingira, ili kuweka Jiji la Dar es Salaam katika hali ya usalama.