Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
KAMATI YA SIASA WILAYA YA UBUNGO YAIPA KONGOLE DAWASA UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI MSUMI
25 Feb, 2026
KAMATI YA SIASA WILAYA YA UBUNGO YAIPA KONGOLE DAWASA UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI MSUMI

Kamati ya Siasa Wilaya ya Ubungo ikiongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya hiyo, Mheshimiwa Rogat Mbowe wameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kasi ya utekelezaji wa mradi wa maji Msumi ikisema mradi huo unakwenda kuwa muarobaini wa changamoto ya maji Mtaa wa Msumi.

Hayo yameelezwa katika ziara ya Kamati ya Siasa Wilaya ya Ubungo kukagua miradi ya maendeleo katika Wilaya hiyo ambapo mradi wa maji Msumi ulitembelewa na kukaguliwa.

"Natoa shukrani zangu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutenga fedha nyingi kutekeleza mradi huu, lakini zaidi niwapongeze DAWASA katika miradi inayotekelezwa kwa kasi kubwa basi huu ni wa mfano, ni wazi sasa wananchi wa Msumi wanaenda kuondokana na adha ya maji," amesema Mbowe.

Mbowe amesema Chama kitaendelea kuwa karibu na DAWASA kusimamia maendeleo ya mradi huu ili kuhakikisha kasi hii haipungui, huku akiwataka DAWASA kufanya kazi usiku na mchana kukamilisha kazi iliyobaki.

Kwa upande wake, Mshahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo na Diwani wa Kata ya Goba, Mheshimiwa Lawrence Mlaki amesema mradi huu unakwenda kumaliza tatizo la maji katika mtaa wa Msumi na maeneo jirani huku akipongeza kasi ya utekelezaji wake na kutaka miradi ya maendeleo sehemu mbalimbali kuwa na kasi ili wananchi waanze kunufaika na uwekezaji wa Serikali inayofanya.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mhandisi Azizi Namanga amesema kwa sasa ujenzi wa kituo cha kusukuma maji umefikia asilimia 65 na wamekwishapokea vitu vyote vya muhimu kama vile transfoma ya umeme pamoja na pampu ya kusukuma maji.

"Mradi unahusisha ulazaji wa mtandao wa bomba za maji kwa umbali wa km 14.96, ujenzi wa tenki lenye ukubwa wa lita 500,000 katika Mnara wa Mita 12 pamoja na ujenzi wa vizimba 12 vya kuchotea maji, mradi utanufaisha zaidi ya wakazi 47,000 utakapokamilika," amesema Mhandisi Namanga