KARIAKOO, UPANGA ZANUFAIKA NA UKARABATI WA MIUNDOMBINU YA MAJITAKA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea na kazi za kuboresha miundombinu ya majitaka katika maeneo ya Kariakoo na Upanga, Wilaya ya Ilala, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa huduma na kuzuia uchafuzi wa mazingira unaotokana na kutiririka kwa majitaka mitaani.
Kazi zinazoendelea zinahusisha ukarabati wa chemba za majitaka zilizoharibika, ujenzi wa mifuniko mipya ya chemba pamoja na usafishaji wa njia za kupitisha majitaka ili kuhakikisha mfumo huo unafanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza wakati wa utekelezaji wa kazi hizo, Msimamizi wa Miundombinu ya Majitaka DAWASA, Mhandisi Baraka Mpala, amesema Mamlaka imejipanga kuhakikisha miundombinu ya majitaka inalindwa na kuendelea kutoa huduma kwa viwango vinavyohitajika.
“Katika maeneo yote yenye mtandao wa majitaka ikiwemo Kariakoo, Ilala, Sinza, Mwenge na Mikocheni, tumeweka timu zinazofanya kazi saa 24 kushughulikia changamoto mbalimbali za majitaka. Tunawasihi wananchi kuwa walinzi wa miundombinu hii na kuacha kutupa taka ngumu kwenye mifumo ya majitaka kwani husababisha kuziba na kuharibu miundombinu,” amesema Mhandisi Mpala.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kufuata taratibu rasmi za kuunganishwa kwenye mtandao wa majitaka badala ya kufanya maunganisho holela, ambayo mara nyingi husababisha uharibifu wa miundombinu na kupunguza ufanisi wa huduma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kariakoo Magharibi, Ndugu Said Omary, ameishukuru DAWASA kwa mwitikio wa haraka katika kutatua changamoto zinazoripotiwa na wananchi.
“DAWASA imekuwa mstari wa mbele kushughulikia changamoto za majitaka kila zinapojitokeza. Tunatoa rai kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu hii muhimu ili kuepusha milipuko ya magonjwa yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira, ikiwemo kipindupindu,” amesema.
DAWASA imeendelea kuimarisha huduma za usafi wa mazingira kwa kufanya maboresho ya mara kwa mara katika miundombinu ya majitaka, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha mazingira safi na salama kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
