WATUMISHI WAKUMBUSHWA USIMAMIZI AFYA NA USALAMA MAHALA PA KAZI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imewakumbusha watumishi kuzingatia kanuni na miongozo ya afya na usalama mahala pa kazi ili kupunguza ajali na madhara yanayoweza kujitokeza kazini yatakayoathiri utendaji kazi.
Hayo yamebainishwa wakati wa mafunzo elekezi ya kuongeza uelewa kuhusu afya na usalama mahala pa kazi yaliyotolewa na Wakala wa Usalama na Afya mahala pa kazi (OSHA) ili kuwajengea uwezo wa kutambua na kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa majukumu.
Kaimu Mkurugenzi Rasilimali watu na Utawala DAWASA, Ndugu Stella Fumbuka amesisitiza umuhimu wa watumishi kuzingatia kanuni na miongozo ya afya na usalama ili kupunguza ajali na madhara yanayoweza kujitokeza kazini.
"Uelewa wa huduma ya kwanza na matumizi ya vifaa vya kuzimia moto ni nyenzo muhimu zinazoweza kuokoa maisha na mali wakati wa matukio ya dharura, kwa kujilinda tutaepusha hasara kwa Mamlaka na hivyo kuchochea huduma bora kwa wananchi," amesema Ndugu Fumbuka.
Afisa Mafunzo kutoka Wakala wa Usalama na Afya mahala pa kazi (OSHA), Ndugu Erick Mororo amesema msingi wa usalama mahala pa kazi ni Sheria Na. 5 ya Mwaka 2003 inajulikana kama Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ambayo inasimamiwa na OSHA Kwa lengo la kulinda usalama, usalama na ustawi wa watumishi wakiwa kazini.
"Kwanza ni jambo jema kukutana na kukumbushana masuala haya muhimu lakini pia niwaase watumishi kuchukua tahadhari mahala pa kazi pamoja na kutoa taarifa wanapoona viashiria vya hatari, hii itasaidia kuwalinda lakini pia hata ambao sio wananchi," amesema ndugu Mororo.
