Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
KAYA 4,700 KUNUFAIKA NA KISIMA MIPEKO, DAWASA YAINGIA KAZINI
05 Oct, 2026
KAYA 4,700 KUNUFAIKA NA KISIMA MIPEKO, DAWASA YAINGIA KAZINI

Wananchi wa vijiji vya Mwanambaya na Mipeko, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, wanatarajiwa kupata huduma ya maji kwa uhakika zaidi baada ya Mamlaka ya Majisafi an usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kuanza uchimbaji wa kisima kipya kinacholenga kuhudumia zaidi ya kaya 4,700.

Kisima hicho kinachojengwa eneo la Mwanambaya, Kata ya Mipeko, kinagharimu Sh milioni 180 na kinatarajiwa kukamilika Oktoba 2026, kikihusisha uchimbaji na ufungaji wa pampu.

Msimamizi wa kazi hiyo, Mhandisi Aziz Namanga, amesema kisima hicho kitaongeza huduma kutoka kaya 800 zinazohudumiwa na kisima kilichopo hadi zaidi ya kaya 4,700 katika vijiji hivyo.

Amesema hatua hiyo inatekelezwa kufuatia maelekezo ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, baada ya kubainika kuwa chanzo cha sasa hakikidhi mahitaji ya wananchi.

Diwani wa Kata ya Mipeko, Adil Hassan Kinyenga, amesema wananchi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya maji tangu mwaka 2021, hivyo kuanza kwa uchimbaji huo kumewapa matumaini ya kupata huduma karibu na makazi yao.

Ameiomba DAWASA kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa weledi na kukamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma hiyo.

Mkazi wa Mwanambaya, Nasra Miraji, amesema adha ya maji imekuwa ikiwasumbua wananchi kwa muda mrefu na kwamba kukamilika kwa kisima hicho kutawasaidia kupata huduma kwa urahisi zaidi.

Uchimbaji huo ni sehemu ya hatua za DAWASA kuongeza vyanzo vya maji na kukidhi mahitaji ya wananchi katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma.