KUNDO: BWAWA LA KIDUNDA MUHIMU KWA USALAMA WA MAJI DAR NA PWANI
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Andrew Kundo, amesema kukamilika kwa mradi wa Bwawa la Kidunda kutaongeza usalama wa maji na kuchochea shughuli za kiuchumi na uwekezaji katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Kundo amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, akieleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji na kuwataka wakandarasi na wasimamizi kuongeza juhudi ili mradi ukamilike kwa wakati.
Amesema bwawa hilo linatarajiwa kuhifadhi lita bilioni 190 za maji, ambazo zitakuwa sehemu ya miundombinu muhimu katika kukuza uchumi wa mikoa hiyo na kutekeleza kwa vitendo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Maji haya lita bilioni 190 yatakayohifadhiwa hapa yatakuwa miundombinu ya msingi sana katika ukuaji wa uchumi wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro,” amesema Kundo.
Ameeleza kuwa pamoja na ujenzi wa bwawa, ulinzi wa vyanzo vya maji unapaswa kupewa kipaumbele kwa kuhifadhi misitu na maeneo oevu, kudhibiti shughuli zinazoharibu vyanzo vya maji na kuwawezesha wananchi kupata shughuli mbadala za kiuchumi.
Diwani wa Kata ya Mkulazi, Abeid Mnyanga, amesema wananchi wa eneo hilo tayari wananufaika na mradi kupitia ajira na miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara, huku akieleza kuwa ushirikiano kati ya wananchi, Serikali ya mtaa na watekelezaji wa mradi ni mzuri.
Mwenyekiti wa Bodi ya DAWASA, Mhandisi Romanus Mwang’ingo, amesema DAWASA inaendelea kufuatilia kwa karibu kazi za Mhandisi Mshauri na Mkandarasi ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa manufaa yaliyokusudiwa.
Mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 329 umefikia asilimia 65 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Juni 2027, huku ukusanyaji wa maji katika bwawa ukitarajiwa kuanza Desemba 2026.
