KILIO CHA MAJI CHAMALIZWA KILUVYA

Wakazi wa Kata ya Kiluvya, Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani wameondokana na adha ya muda mrefu ya ukosefu wa huduma ya maji na gharama kubwa waliyokuwa wakitumia kuipata baada ya kukamilika kwa mradi wa maboresho ya huduma ya maji NSSF.
Mradi huo umetekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa gharama ya Shilingi milioni 37 na unahudumia mitaa ya Mji Mpya, Tondorini, Mwanakondoo, Kwa Msigwa pamoja na Makurunge.
Wakizungumzia ahueni waliyoipata baada ya kukamilika kwa mradi huo, wananchi wa mtaa wa Mji Mpya wameipongeza DAWASA kwa maboresho katika mradi huo kwani sasa wanapata huduma ya maji yenye uhakika.
"Hapo kipindi cha nyuma ilitulazimu kuacha shughuli zetu za kimaendeleo kama ufugaji na ujenzi kwa adha ya kukosa huduma ya maji, lakini kwa zaidi ya wiki sasa huduma ya maji imeimarika na shughuli tulizozisimamisha sasa zinaendelea tena," amesema John Simba, mkazi wa mtaa wa Mji Mpya.
Simba ameitaka DAWASA kusimamia vyema hali hiyo ya upatikanaji wa maji kwasasa iwe endelevu ili wakazi wa Kiluvya waendelee kunufaika na huduma ya maji.
Kwa upande wake, Paul Sadat, Mwenyekiti wa Mtaa Mji Mpya amesema kukamilika kwa mradi huo na kuanza kufanya kazi kunawapunguzia gharama kubwa za maisha wakazi wa eneolake.
Amesema awali walilazimika kununua maji kwa gharama kubwa ya Shilingi 60,000 kwa pipa moja lenye ujazo wa lita 1000, huku akiomba DAWASA kuendelea kufuatilia kwa karibu kila mwananchi aliyekuwa hapati huduma aweze kuipata.
Mhandisi Mkashida Kavishe, Meneja wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma Kibamba amesema hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa sasa inaridhisha katika Kata ya Kiluvya kulinganisha na awali kabla ya maboresho ya mradi.
"Tulipokea mradi huu kutoka NSSF, ukihitaji maboresho makubwa ambapo awali ulikuwa kwaajili ya kuhudumia viwanja vya NSSF pekee, wakazi wa maeneo haya walikuwa wakipata huduma ya maji kwa msukumo mdogo mara moja kwa wiki na wengi wao walikuwa hawapati kabisa huduma.
“Tumefanya maboresho na sasa huduma ya maji inapatikana ya uhakika sio tu katika viwanja vya NSSF bali hadi mitaa ya jirani," amesema Mhandisi Kavishe.
Kavishe amesema mradi wa maji NSSF unahusisha ulazaji wa bomba zenye ukubwa wa inchi 4 kwa umbali wa kilomita 1.4 na inchi 3 kwa mita 600 pamoja tenki la kuhifadhi maji lita 500,000.