Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
KILIO CHA MAJI CHAMALIZWA STAKISHARI
31 Jul, 2025
KILIO CHA MAJI CHAMALIZWA STAKISHARI

Kilio cha muda mrefu cha wakazi wa mtaa wa Stakishari, Kata ya Kipawa, wilayani Ilala cha ukosefu wa majisafi sasa kimegeuka kicheko baada ya huduma hiyo kupatikana mlangoni mwao.

Hii ni baada ya ya kukamilika kwa Mradi wa Usambazaji Maji Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo) ambao unahudumia majimbo matano ya uchaguzi ya Ukonga, Segerea, Ubungo, Temeke na Kisarawe.

Mradi huo umetekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa gharama ya Shilingi Bilioni 36.9.

Ndugu Clara Jame, mkazi wa mtaa wa Stakishari amesema adha waliyoipata kina mama majumbani siku za nyuma kutokana na ukosefu wa huduma ya majisafi, sasa imekwisha na shughuli zote za majumbani zinafanyika kwa wepesi.

"Kipindi kile tunalazimika kwenda umbali mrefu kutoka eneo hili kwenda kufuata maji, na ukiangalia maji tuliyokuwa tunatumia yalikuwa maji ya kisima na ni ya chumvi, naipongeza DAWASA kwa kazi kubwa mliyoifanya kutuletea majisafi na salama," amesema James.

Naye Gaudence Mwaikibaki, mkazi wa mtaa wa Stakishari amesema kukamilika kwa mradi huu na kuimarika kwa huduma ya maji katika mtaa wake ni ishara ya kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.

"Hapo awali tulikuwa tukitegemea chanzo cha maji ambacho ni kisima lakini kupitia uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi sasa katika mtaa wa Stakishari, maji ni mwa! mwa! mwaa!," amesema Mwaikibaki.

Kwa upande wake, Ibrahim Mavura, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Stakishari ameipongeza DAWASA kwa utekelezaji wa mradi huo kwani sasa huduma ndani ya mtaa wake imekuwa imara ikilinganishwa walipokuwa wakitegemea kisima cha maji kama chanzo chao.

Amesema awali walilazimika kununua maji kwa gharama kubwa, na maji hayo yalikuwa ya kisima na yenye chumvi ambayo sio salama kwa matumizi ya binadamu, huku akiomba DAWASA kuendelea kufuatilia ili kuhakikisha kila mwananchi aliyekuwa hapati huduma aweze kuipata.

"Hapo awali tulikuwa tukitegemea kisima kama chanzo pekee cha maji kwa ajili yetu, tunaishukuru na kuipongeza DAWASA kwa mradi huu na sasa nitoe rai kwa wananchi kuendelea kuwasilisha maombi ili kuunganishwa rasmi katika mtandao na kuanza kunufaika ma mradi," amesema Mavura.