KISUKURU, GOLANI NA MSUMI WAPEWA KIPAUMBELE NA DAWASA
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire ametembelee maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam kujionea upatikanaji wa Maji na kuweka mikakati ya kumaliza changamoto mbalimbali za kihuduma katika maeneo hayo.
Mhandisi Bwire ametembelea maeneo ya Kisukuru Banebane, Golani, pamoja na Msumi ambapo mipango ya kutatua changamoto ya majisafi katika maeneo hayo yamewekwa bayana.
"Tumekagua maeneo yenye huduma na ambayo bado ni changamoto lakini, pia tumejiwekea mipango ya kutatua changamoto hizo, Katika eneo la Kisukiri tutaenda kuangalia uwezekano wa kukarabati tenki la kuhifadhi maji Kisukuru Magonza liweze kutumika tena kwa Wananchi wa maeneo hayo sambamba na uchimbaji wa visima, kwa eneo la Golani na Msumi tutaenda kujenga vituo vya kusukuma maji (booster station) ili wananchi waimarishiwe upatikanaji wa huduma ya majisafi," amesema Mhandisi Bwire.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Bwire ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa Usafi wa Mazingira Mbezi Beach na kuridhishwa na kazi ya utekelezaji wake ambapo kazi ya mtambo ya ujenzi wa mtambo wa kuchakata majitaka umefikia asilimia 40.
"Kazi kubwa imefanyika na inaendelea kufanyika, nimsisitize Mkandarasi na Mhandisi Mshauri kuendelea kusimamia mradi ukamilike kwa wakati bila kutokea changamoto zinazoweza kuepukika," amesema Mhandisi Bwire.
