Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MABOMBA CHAKAVU MINAZINI - MAKUMBUSHO YAANZA KUBADILISHWA
04 Oct, 2026
MABOMBA CHAKAVU MINAZINI - MAKUMBUSHO YAANZA KUBADILISHWA

Wananchi wa Mtaa wa Minazini, Kata ya Makumbusho, Kinondoni, wanatarajiwa kupata huduma ya maji yenye msukumo zaidi baada ya DAWASA kuanza kubadilisha mabomba chakavu katika eneo hilo.

Kazi hiyo inatekelezwa kupitia Mradi wa Maji Bukene Mwananyamala, ambapo bomba mpya za ukubwa wa inchi nane zitalazwa kwa umbali wa kilomita 1.2. Hadi sasa, mita 500 za bomba hizo zimekwishalazwa.

Mhandisi wa Miradi Mkoa wa Kihuduma Kinondoni, Gloria Filipatali, amesema kazi hiyo inalenga kuboresha mtandao wa usambazaji na kuongeza msukumo wa maji kwa wananchi.

“Kazi hii inahusisha ulazaji wa bomba za ukubwa wa inchi nane kwa umbali wa kilomita 1.2. Mpaka sasa tumeshawalaza mita 500. Lengo kubwa ni kuongeza msukumo wa maji na kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi,” amesema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Minazini, Zunda Muhani, amesema mabomba yaliyokuwepo yalikuwa yamechakaa kutokana na kuwa ya muda mrefu, hivyo hatua ya kuyabadilisha itasaidia kuimarisha huduma.

“Tunawashukuru DAWASA kwa kuona umuhimu wa kubadilisha mabomba haya ambayo yalikuwa ya zamani sana. Tunaamini mabomba mapya yatasaidia kuongeza msukumo wa maji na kuboresha huduma kwa wananchi wa Minazini,” amesema Muhani.

Mkazi wa Minazini, Avijawa Katanga, amepongeza hatua hiyo, akisema uboreshaji wa miundombinu ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa upatikanaji wa maji.

DAWASA inaendelea kuboresha miundombinu ya usambazaji kwa kuondoa mabomba chakavu na kuweka mifumo mipya yenye uwezo wa kusaidia utoaji wa huduma kwa ufanisi zaidi.