Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
WAKAZI ZAIDI YA 400 GONGO LA MBOTO WABORESHEWA HUDUMA YA MAJI
04 Oct, 2026
WAKAZI ZAIDI YA 400 GONGO LA MBOTO WABORESHEWA HUDUMA YA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kupitia mafundi wa Mkoa wa Kihuduma wa Ukonga, inaendelea na maboresho ya miundombinu ya maji katika eneo la Gongo la Mboto Jeshini ili kuongeza upatikanaji wa maji na kuboresha huduma kwa wateja zaidi ya 400 waliopo katika maeneo husika.

Kazi hiyo inayotekelezwa katika makutano ya bomba kuu eneo la Gongo la Mboto Jeshini inahusisha kazi ya ufungaji toleo la bomba jipya lenye kipenyo cha inchi 4 kutoka kwenye bomba kuu lenye kipenyo cha inchi 16 kwenda kwenye mtandao wa usambazaji maji kwa wateja.

Kukamilika kwa matengenezo hayo kutaboresha huduma ya upatikanaji wa maji na kunufaisha wakazi wa maeneo ya Kampala University, St. Thomas, Marangu, Serikali ya Mtaa, Bumila, Kaza Roho, Markaz, Mazizini na Mzambarauni.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za DAWASA za kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa jamii, kupunguza changamoto za upatikanaji wa maji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.