MADIWANI ILALA WAPONGEZA KASI UTEKELEZAJI MRADI WA KIDUNDA

Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam imeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya maamuzi makubwa ya kuanza kutekeleza mradi wa kihistoria wa Bwawa la Kidunda ambalo litasaidia kwa sehemu kubwa kukabiliana na upungufu wa maji kwa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Akizungumza wakati wa ziara katika Bwawa hilo, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Saad Kumbilamoto amesema kuwa hatua ya utekelezaji wa mradi huu ni ya muhimu kwa kuwa inaleta tija kwa wananchi wote walengwa wa Dar es Salaam na Pwani.
"Fursa hii tuliyoipata ya kutembelea mradi huu imetupa funzo kubwa kwetu sisi Madiwani ya kujua na kuona kazi kubwa ambayo Serikali ya Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan inafanya kwa wananchi wake hususani katika Sekta ya maji," amesema Mhe. Kumbilamoto.
"Tumefurahishwa na ziara hii katika miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, imekuwa na tija kubwa kwetu hususani kwa kujifunza jitihada zinazofanywa katika miradi ya maji, lakini pia kuwaandaa Madiwani kuwa mabalozi wazuri katika kuhamasisha utunzaji mzuri wa vyanzo na miundombinu ya maji ili huduma iweze kupatikana muda wote," amesema Mhe. Kumbilamoto.
kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kitunda Mhe. Victor Vedasto ameahidi kuwa balozi mzuri wa ulinzi wa miundombinu ya maji kwani gharama zinazotumika katika utekelezaji wa mradi huu ni kubwa, na lengo la Serikali la kuwapatia wananchi huduma bora linapaswa kutimia.
"Nimeona jinsi utekelezaji wa Bwawa hili ulivyo mkubwa na unaotekelezwa kwa gharama kubwa kwa lengo la kuwezesha wananchi wapate huduma bora na kwa wakati, hivyo ni vyema kwa wananchi wetu kuwa na uchungu pale anapoona kuna uharibifu," amesema Mhe Vedasto.
Msimamizi wa mradi, Mhandisi Christian Christopher ameishukuru Serikali kwa maamuzi makubwa iliyofanya ya kuamua kutekeleza mradi huu wa muda mrefu.
"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji na DAWASA kama wasimamizi wa mradi huu tunaahidi kuendelea kusimamia ipasavyo maagizo na ukamifu sahihi wa utekelezaji wa mradi huu ili kuhakikisha kazi hii iliyoanza inakamilika ndani ya muda uliopangwa," amesema Mhandisi Christopher.
Ujenzi wa Mradi wa Bwawa la kidunda unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 329 wenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi kwa kipindi chote cha mwaka.