MADIWANI ISAIDIENI DAWASA KUDHIBITI UPOTEVU WA MAJI - RC KUNENGE
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abuukakar Kunenge amewataka Waheshimiwa Madiwani wa Mkoa wa Pwani kuisaidia Serikali kupiti Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)katika mapambano ya kukabiliana na changamoto ya upotevu wa majisafi inayoigharimu Mamlaka kwa kiasi kikubwa.
Amesema kuwa upotevu wa maji ni changamoto inayotokea katika makazi ya watu na inawezekana kabisa kudhibitiwa kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia upotevu wa maji.
Amesema kuwa katika maeneo mengine, kuna wananchi wasio waaminifu wanaotoboa mabomba ili wajipatie maji kiurahisi, hii siyo sawa. Hivyo nguvu ya ziad inahitajika kukabiliana na hali hii.
"Tunapaswa wote kuwa na nia moja ya kuhakikisha tunaweka nguvu katika kupunguza kiwango cha maji yanayopotea mitaani, kwa kuwa mabalozi kwa wananchi na kutoa elimu kwao juu ya umuhimu wa kudhibiti maji haya yanayopotea na kuona thamani yake na kuyatunza," amesema Mhe. Kunenge.
"Tunapaswa kuisaidia DAWASA kudhibiti upotevu wa maji kwa kuwa, gharama inayotumika ya kuzalisha maji ni kubwa kuliko mapato yanayopatikana kupitia ulipaji wa bili, maji mengi yanapotea lakini mapato yanahohitika kuboresha huduma ni machache," ameeleza Mhe. Kunenge.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa wananchi wanapaswa kuelewa kuwa uzalishaji wa maji ni hatua inayohusisha vitu vingi, na Mamlaka inajitahidi kuhakikisha maji yanayozalishwa yanakuwa katika ubora unaotakiwa.
Amesema kuwa wakati mwingine huwa kunatokea kuchafuka kwa maji hususani katika kipindi cha msimu wa mvua, hivyo Mamlaka inachokifanya ni kuhakikisha licha ya mabadiliko ya hali ya hewa lakini wananchi wapate maji yaliyo na ubora unaotakiwa.
"Hivyo mwanzoni mwamsimu wa mvua palitokea changamoto ya maji kubadilika lakini kwa sasa hiyo imeisha na huduma inaendelea kutolewa katika viwango vya ubora wa hali ya juu," ameeleza Mhandisi Bwire.
Ameongeza kuwa kwa sasa pampu mpya zimeshafika na hii ni ishara kuwa kwa sasa uzalishaji wa maji unaenda kuimarika kwa kiasi kikubwa na hapatakuwa na kusuasua kwa uzalishaji wa maji kama awali uliosababishwa na ubovu wa pampu za kuzalisha na kusukuma maji.
