MADIWANI KINONDONI WAUNGA MKONO MIPANGO YA KUDHIBITI UPOTEVU WA MAJI
Madiwani wa Wilaya ya Kinondoni wameahidi kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kudhibiti upotevu wa maji unaosababishwa na wizi na mivujo ya mabomba, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Madiwani hao wa kata zote 20 wametoa ahadi hiyo katika kikao kazi na DAWASA kilicholenga kujenga uelewa kuhusu usimamizi wa huduma za maji, utekelezaji wa miradi na nafasi ya viongozi wa maeneo katika kulinda miundombinu na kudhibiti upotevu wa maji.
Akifungua kikao hicho, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Warda Abdallah, ameishukuru DAWASA kwa kuwapa madiwani fursa ya kutembelea miradi, vyanzo vya maji na Mtambo wa Uzalishaji Maji wa Ruvu Chini ili kujionea na kujifunza kuhusu jitihada za kuboresha huduma.
Amesema ushirikiano kati ya DAWASA, madiwani na watendaji wa kata ni muhimu katika kupambana na wizi wa maji na mivujo ya mabomba, huku akiwataka viongozi hao kuhamasisha wananchi kutoa taarifa na kuunga mkono shughuli za mamlaka hiyo.
“Nawapongeza DAWASA kwa jitihada za kuboresha huduma ya maji katika Wilaya ya Kinondoni. Ni muhimu kuendeleza ushirikiano katika kudhibiti upotevu wa maji unaosababishwa na mivujo na wizi wa maji ili huduma iendelee kuimarika na kuwafikia wananchi wengi zaidi,” amesema Warda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangingo, amesema upotevu wa maji ni changamoto kubwa kwa mamlaka hiyo na kwamba mafanikio ya kuidhibiti yanategemea pia ushirikiano wa viongozi wa maeneo na wananchi.
Amesema madiwani na watendaji wa kata wana nafasi muhimu ya kuhamasisha jamii kulinda miundombinu ya maji na kutoa taarifa kuhusu vitendo vya wizi pamoja na mabomba yanayovuja.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amesema kikao hicho kinalenga kuwajengea madiwani uelewa kuhusu usimamizi wa huduma za maji na wajibu wao katika kufuatilia mipango ya kuboresha huduma katika kata zao.
Amesema DAWASA inaendelea kuboresha huduma kupitia mpango wa miaka mitano, hivyo ushirikiano wa madiwani ni muhimu katika kutoa taarifa na mapendekezo yatakayosaidia kukabiliana na wizi wa maji na mivujo ya mabomba.
Akichangia katika kikao hicho, Diwani wa Kata ya Magomeni amesema wizi wa maji bado ni changamoto katika eneo hilo, licha ya baadhi ya wahusika kukamatwa na kutozwa faini. Ameeleza kuwa baadhi yao wamekuwa wakirejea katika vitendo hivyo baada ya kuchukuliwa hatua.
Ameiomba DAWASA kushirikiana na wadau wengine kutafuta suluhu ya kudumu ya kukomesha wizi huo, akisema kurudiwa kwa vitendo hivyo kunadhoofisha juhudi za kuboresha upatikanaji wa maji kwa wananchi.
Kabla ya kikao hicho, madiwani walitembelea miradi na vyanzo vya maji vilivyopo Kinondoni pamoja na Mtambo wa Uzalishaji Maji wa Ruvu Chini, kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji na usambazaji wa maji na hatua zinazochukuliwa na DAWASA kuboresha huduma.
