MADIWANI WAIPONGEZA DAWASA, MRADI KUPUNGUZA GHARAMA ZA MAJITAKA
Madiwani wa Wilaya ya Kinondoni , Mkoani Dar es salaam wamepongeza utekelezaji wa mradi wa kisasa wa uondoshaji na uchakataji wa majitaka katika maeneo ya Mbezi Beach na kuomba huduma kama hiyo isambazwe katika maeneo mengine ili kupunguza gharama za wananchi za kuondoa majitaka majumbani.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwananyamala, amesema mradi huo ni hatua muhimu katika kuboresha usafi wa mazingira na kuifanya Dar es Salaam kuwa mji wenye mifumo bora ya uondoshaji majitaka.
Mnyonge ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya madiwani wa kata mbalimbali za Wilaya ya Kinondoni, iliyolenga kukagua hali ya uzalishaji na usambazaji wa maji pamoja na utekelezaji wa huduma za usafi wa mazingira. Ziara hiyo imeratibiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amesema baadhi ya maeneo ya Mbezi Beach yanakabiliwa na changamoto ya uondoshaji wa majitaka kutokana na hali ya kijiografia, ikiwamo uwepo wa maji juu ya ardhi, jambo linalowalazimu wananchi kutumia gharama kubwa kuyaondoa majitaka katika makazi yao.
Amesema mradi huo unalenga kupunguza gharama hizo kwa kuweka mfumo wa kisasa utakaorahisisha ukusanyaji na uondoshaji wa majitaka.
Diwani wa Kata ya Kijitonyama, Amani Bandale, amesema uwekezaji huo ni muhimu katika kuboresha afya ya jamii na mazingira, huku akiiomba Serikali kupitia DAWASA kuendeleza miradi kama hiyo katika maeneo mengine ili wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma za usafi wa mazingira.
Mradi wa uondoshaji na uchakataji wa majitaka wa Mbezi Beach unalenga kuhudumia wakazi wa Kata za Mbezi Beach, Kawe, Kunduchi, Mbezi Juu na Wazo. Utekelezaji wake unasimamiwa na DAWASA, huku kazi zikifanywa na Kampuni ya Ujenzi ya Beijing kwa kushirikiana na Mhandisi Mshauri Doha Engineering.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.
