Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MAJI CHINI YA ARDHI MKOMBOZI WA HUDUMA KWA WAKAZI DAR NA PWANI
30 Jun, 2026
MAJI CHINI YA ARDHI MKOMBOZI WA HUDUMA KWA WAKAZI DAR NA PWANI

Visima vya maji, vilivyopo chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam DAWASA vimekua chanzo muhimu cha huduma ya maji vikichangia asilimia 9 ya maji yanayozalishwa na kusambazwa kwa wananchi  katika eneo la kihuduma la DAWASA.

DAWASA imeendelea na uboreshaji wa visima katika maeneo mbalimbali ikihusisha ufufuaji wa visima 19 kukidhi mahitaji ya wananchi ambapo hadi sasa jumla ya visima 113 vinafanya kazi katika eneo la kihuduma la Mamlaka.

"Mamlaka inaendelea na jitihada mbalimbali kuhakikisha visima hivi vinahudumia wananchi, mpaka sasa tumefufua jumla ya visima 19 ambavyo tumeviunganisha katika mifumo ya majisafi yakutoa huduma kwa wananchi moja Kwa moja majumbani, lakini pia wananchia ambao hawana mfumo wa majisafi wanaweza kuchota maji katika visima hivyo kwa utaratibu maalumu uliowekwa" ameeleza Mhandisi Polycarp Choma. 

Polycarp amesema kuwa lengo la visima hivi si tu kutumka pindi kunapokua na changamoto ya maji, Bali vitatumika muda wote kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa muda mrefu na kuendesha shughuli zao za kila siku bila changamoto yeyote.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mburahati Kwa Mrosso ndugu, Raphael Mteka ameeleza kuwa kwasasa wananchi wanapata huduma ya maji kwa bei rafiki, lakini pia kwa umbali mfupi sana kulinganisha na awali kabla ya maboresho ya kisima kufanyika.

Ndugu Zainabu Ally, mkazi wa Mburahati Kwa Jongo ameeleza kuwa wananchi wanapata unafuu wa maisha kupitia maboresho haya ya visima huku gharama za maisha zikishuka kutokana na upatikanaji rahisi wa huduma ya majisafi.

"Tulilazimika kufata maji mabondeni, na muda mwingine kununua maji kwa bei ghali, jambo ambalo kwasasa halipo, tunatumia maji ya kisima chetu hapa yanayopatikana kwa bei rafiki na umbali mfupi sana, tunawashukuru DAWASA kwa utatuzi huu waliotupatia." Ameeleza ndugu Zainabu.