MAKURUNGE YATENGEWA MILIONI 400 UBORESHAJI HUDUMA ZA MAJI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Kisarawe Mkoani Pwani imeweka mkakati wa kuboresha huduma ya maji katika Kitongoji cha Makurunge katika Kata ya Kiluvya na maeneo mengine yenye changamoto ya upatikanaji wa maji.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Aidan Kitale, amefanya ziara ya kukagua hali ya huduma katika maeneo ya Kiluvya, Makurunge na Mwanakondoo, ikiwa ni sehemu ya kubaini changamoto za usambazaji na hatua za kuzitatua.
Amesema ziara hiyo imewezesha viongozi kuona hali halisi ya upatikanaji wa maji na changamoto za miundombinu, ikiwemo kutoka kwenye chanzo cha bomba la inchi 10 linalopeleka maji katika Tenki la NSSF, Mwanakondoo hadi Makurunge.
“Tumetembelea maeneo mbalimbali na kujionea hali ya upatikanaji wa maji pamoja na kubaini changamoto zilizopo na kuziwekea mkakati wa kuzitatua,” amesema Kitale.
Amesema Halmashauri na DAWASA wamekubaliana kuchagiza utekelezaji wa miradi ya maji iliyosanifiwa ili kuongeza upatikanaji wa huduma katika maeneo yenye changamoto.
Kwa upande wake, Meneja wa DAWASA Kisarawe, Mhandisi Sirila Josephat, amesema katika Kitongoji cha Makurunge wamekubaliana kuongeza nguvu katika kuanza utekelezaji wa mradi uliosanifiwa kwa gharama ya Sh milioni 438.
Amesema mradi huo unahusisha kubadilisha bomba la zamani la inchi 2.5 na kuweka bomba la inchi nne kwa urefu wa kilomita 11, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa kusambaza maji kwa wakazi wa eneo hilo.
Mhandisi Sirila amesema utekelezaji wa mradi huo pamoja na mingine iliyosanifiwa utasaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji na usambazaji wa maji kwa wananchi wa maeneo yenye huduma hafifu.
