MATENGENEZO BOMBA KUBWA MPIJI YAFIKIA 80%
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea na kazi ya matengenezo kinga katika bomba kuu la inch 72 katika eneo la mto Mpiji, Wilaya Kinondoni ambapo yamefikia asilimia 80.
Akizungumzia maendeleo ya kazi hiyo, Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji DAWASA, Mhandisi Ndele Mengo amesema tayari wamekwisha kamilisha kazi ya ulazaji wa bomba hilo na kuunganisha katika maungio yake mapya.
"Kilichobaki sasa baada ya kukamilisha kuchomea maungio ya bomba ni kuongeza uzalishaji ili tuweze kujaza maji katika kiwango kinachotakiwa katika bomba na kufanya majaribio na baadae kuruhusu huduma kurejea kwa wananchi" amesema Mhandisi Ndele
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Boko Chama, Ndugu Belico Mkute amebainisha kuwa mtaa wake unahudumia na bomba hilo ambapo walipata taarifa za kupungua kwa huduma ya maji kutokana na matengenezo kinga kupitia vyombo habari na kuwataarifu wananchi wake.
"Ni kweli tulipokea taarifa upungufu wa huduma kwa muda wa Siku nne lakini katika mtaa wetu tumeendelea kupata huduma ya maji japo sio katika msukumo mkubwa kama awali lakini yanapotoka tumeendelea kuhifadhi hadi matengenezo yatakapokamilika” amesema Mkute
Mkazi wa Mtaa wa Boko Chama, Ndugu Gabriel Kolimba amebainisha kuwa alipata taarifa za kuhusiana na upungufu wa huduma ya maji kupitia makundi Sogozi ya wateja na Mamlaka ambapo muda wa upatikanaji wa huduma kwa kipindi hicho umepungua tofauti na awali, aidha ameishukuru Mamlaka kwa kutositisha kabisa huduma kama walivyotarajia awali.
"Matengenezo tunaona ni sehemu muhimi katika kuimarisha huduma na haswa tulivyoambiwa lengo kuu ni kuchukua tahadhari ya bomba kusombwa kwa miundombinu kuelekea mvua kubwa za Elnino" amesema Kolimba
Mamlaka imeendelea kuwasihi wananchi wanahudumiwa na bomba hilo katika ukanda wa Bagamoyo hadi Ilala kuendelea wavumilivu katika kipindi hichi cha matengenezo kinga kinachoendelea na huduma inatarajia kurejea kwa wakati kwa muda uliyokuwa umebainishwa awali.
