MHANDISI BWIRE ACHAGIZA UKAMILISHWAJI WA MIRADI KWA WAKATI

Ataka Huduma bora kwa Wananchi kupitia ufanisi wa miradi ya kimkakati
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, mhandisi Mkama Bwire ametoa maelekezo kwa wasimamizi wa miradi ya majisafi ya Mamlaka kuhakikisha utekelezaji wa miradi muhimu unaenda sambamba na kasi ya mahitaji ya wananchi katika maeneo yao husika.
Mhandisi Bwire ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua eneo la ujenzi wa kituo cha kusukuma maji (booster station), eneo la ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji la lita milioni 6 katika eneo la Pangani, pamoja na tenki la kuhifadhi maji katika eneo la Vikawe, Mapinga ambalo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kusambaza maji kutoka Makongo hadi Bagamoyo.
Mhandisi Bwire amewasisitiza wasimamizi wa miradi ya majisafi kuhakikisha kuwa kazi zote zinakamilika kama ilivyopangwa kwenye mkataba wa mradi, akisisitiza kuwa kuchelewa kwa miradi hiyo kunaathiri maisha ya wananchi moja kwa moja.
"Ni muhimu taratibu za utekelezaji wa miradi ziheshimiwe na kazi ziendelee kwa kasi ili kuleta matokeo chanya katika jamii kama ilivyokusudiwa wakati wa usanifu," amesema Mhandisi Bwire.
Vilevile, ametumia ziara hiyo kuwasisitiza watendaji wa DAWASA wanaosimamia usambazaji wa maji kwa maeneo ya Vikawe Shule, Vikawe Bondeni, Kidimu Miwale na Mkombozi. kupitia tenki la Vikawe kuongeza usimamizi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika kwani ni huduma muhimu kwa maendeleo ya kila mmoja.
"Nisisitize kuongeza usimamizi katika utoaji wa huduma pia kudumisha ushirikiano na Viongozi wa Serikali za Mitaa ambao hutusaidia katika utoaji wa taarifa zinazohusu huduma zetu pamoja na kuhamasisha wananchi," ameeleza Mhandisi Bwire.