Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
MILIONI 280 ZAPELEKA SHANGWE YA HUDUMA ZA MAJI MBOPO
05 Jun, 2025
MILIONI 280 ZAPELEKA SHANGWE YA HUDUMA ZA MAJI MBOPO

Wananchi zaidi ya 200 waunganishwa na huduma na kupata fursa ya kuunganishiwa maji kwa mkopo

Wananchi wa mtaa wa Mbopo, Kata ya Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni wameanza kunufaika na uwekezaji wa fedha za utekelezaji wa mradi wa usambazaji maji Mbopo uliotekelezwa kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam DAWASA uliotekelezwa kwa gharama ya Shilingi Milioni 280. 

Mradi huu ambao umetekelezwa kwa fedha za ndani za Mamlaka, umeanza kunufaisha wananchi wapatao 200 wa Mbopo, na wananchi takribani 302 wamewasilisha maombi ya kuunganishwa maji.

Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa maji Mbopo uliotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndugu Ismail Ali Ussi amesema kuwa mradi huu umeonesha nia ya dhati ya kuwatua ndoo kichwani wananchi wa eneo hili ambao wamekuwa kwenye changamoto ya maji kwa muda mrefu. 

"Tumetembelea na tumejionea namna mradi huu ulivyotekelezwa kwa kuzingatia viwango vyote, ufanisi m umakini katika kila hatua, pia mradi huu umeonesha dhamani ya fedha ambayo Serikali kupitia DAWASA imewekeza kwa lengo la kuwawezesha wananchi kupata huduma ya majisafi," amesema Ndugu Ussi. 

Ndugu Ussi pia amewataka wananchi kuthamini kazi kubwa inayofanywa na Serikali na kuwa mabalozi wazuri wa ulinzi wa miundombinu hii ya maji ili huduma ya maji iwe endelevu na ya uhakika. 

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa mradi huu umetekelezwa kwa gharama ya Shilingi Milioni 280, ikihusisha ulazaji wa mabomba ya mtandao wa kilomita takribani 18 kutoka kwenye tenki la malolo, pamoja na ujenzi wa mnara wa maji ambapo kwa ujumla unanufaisha wakazi 2,000 wa Kata ya Mabwepande, mtaa wa Mbopo. 

Amewataka wananchi waendelee kujitokeza kuunganishiwa maji kwa kuwa kazi ya kulaza mtandao wa mabomba ya kusambaza maji imekamilika, ameongeza kuwa mpaka sasa jumla ya Kaya 156 wamekwisha unganishwa na maji, na wengine takribani 302 wameleta maombi ya kuunganishwa na maji. 

"Hivyo niwaombe wananchi waendelee kujitokeza kuunganishiwa maji na waje wajisajili katika kituo hiki cha DAWASA, na Serikali imetoa unafuu wa kupata maji kwa mkopo na kulipa kidogo kidogo," amesema Mhandisi Bwire. 

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Msingi ya Mbopo Selestine Kindole amesema kuwa anaishukuru sana Serikali kwa kujenga huu mradi kwa kuwa wanafunzi walikuwa wakiteseka namna ya kupata maji kwa ajili ya afya zao. 

"Amewataka wanafunzi kuwa mabalozi wazuri wa utunzaji wa miundombinu ya majisafi ili huduma iweze kuwatunza," amesema Mwl Kindole.