MITA ZA MAJI ZA MALIPO YA KABLA ZAANZA KUTUMIKA RASMI KIGAMBONI

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ndugu Ismail Ali Ussi ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa utekelezaji wa matumizi ya mita za Malipo ya Mita ya Kabla (Pre-paid meters) zilizoanza kutumika kwa Wakazi wa Kigamboni itakayosaidia upatikanaji wa huduma kwa wakati na kupunguza changamoto za kihuduma.
Ndugu Ismail Ali Ussi ametoa pongezi hizo wakati mradi wa Maji ulipotembelea mradi wa usambazaji maji Mtaa wa Kigogo uliotekelezwa na DAWASA.
Amesema kuwa jitihada hizi za Mamlaka kutumia teknolojia hii inaleta tija kubwa kwa wananchi kwa kuwa inarahisisha upatikanaji wa huduma na kuwezesha kutimiza adhma ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi wote.
Ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru Kitaifa umeridhika na utekelezaji wa mradi wa Kigogo uliotekelezwa kwa Gharama ya Shilingi Milioni 780 kwa lengo la kuhudumia wananchi 6,729 wa Mtaa wa Kigogo katika Kata ya Kisarawe II
"Niwapongeze sana DAWASA kwa kuendelea kumsaidia Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha huduma ya majisafi inawafikia wananchi wote kwa uhakika, hii ni fursa kwa wananchi wa Kigogo kunufaika na huduma," amesema Ndugu Usi.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe Halima Bulembo amesema kuwa ujio wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa umeleta unafuu kwa wananchi wa Kata ya Kisarawe II mtaa wa Kigogo ambao wamekuwa kwenye changamoto ya maji kwa muda mrefu.
Akielezea manufaa ya mradi huo Bi Grina Paul, mkazi wa Mtaa wa Kigogo amesema kuwa mradi wa maji unaleta ahueni kubwa kwa kuwa wananchi wengi hawakuwa na huduma ya majisafi na iliyokuwepo ilikuwa kutoka kwa watu binafsi.
"Tunaishukuru sana Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutua ndoo kichwani, hakika mradi huu unaoenda kuleta nafuu ya maisha kwani gharama nyingi tulikuwa tunatumia kununua au kwa wenye visima binafsi," amesema.