Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MRADI WA KISIMA ILALA KUBADILISHA MAISHA YA WAKAZI 2,640
14 Apr, 2026
MRADI WA KISIMA ILALA KUBADILISHA MAISHA YA WAKAZI 2,640

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu Wazo Michael Mwang’onda, ametembelea na kuweka jiwe la msingi mradi wa kisima cha maji kilichopo Ilala Kota Jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo imekuja baada ya kukagua na kuridhishwa na ubora wa utekelezaji wa mradi huo.

Mradi huo unalenga kuboresha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi wa Mtaa wa Ilala Kota, Kata ya Mchikichini, Wilaya ya Ilala na kuwanufaisha wakazi 2,640.
Mradi huo unatakelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa thamani ya Shilingi 164,076,240.18. 

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Ndugu Mwang’onda ameipongeza DAWASA kwa utekelezaji wa mradi huo huku akisema umezingatia viwango vinavyotakiwa na una tija kubwa kwa jamii.

Mradi huo unahusisha uchimbaji wa kisima kirefu chenye kina cha mita 80, ujenzi wa mnara wa tanki lenye ujazo wa lita 10,000, ujenzi wa chemba ya kisima, ufungaji wa pampu na umeme pamoja na ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji umbali wa mita 300 utakaounganisha na mtandao uliopo wa DAWASA.

Mwang’onda amesema Mwenge wa Uhuru umefika Ilala Kota na kukagua mradi huo ambao utekelezaji wake unaendelea vizuri na pindi utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kutoa zaidi ya lita 300,000 za maji kwa siku.Hatua ambayo ameieleza itawanufaisha wakazi wengi wa Mchikichini na maeneo jirani. 

Aidha ameipongeza Serikali kupitia DAWASA kwa mradi huo kwa wananchi wa maeneo hayo ambao kwa kiasi kikubwa utapunguza adha ya wananchi kubeba maji kichwani.

Kwa upande wao, wananchi wa Ilala Kota wameeleza kufurahishwa na mradi huo, wakisema utapunguza kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji, kuboresha usafi na kupunguza gharama za maisha. 

Ndugu Maimuna Mohammed amesema wananchi walikuwa wakipata changamoto kubwa ya maji kwa takribani miaka mitatu, lakini sasa wana matumaini ya kupata huduma hiyo karibu na makazi yao.

Naye Ndugu Salome Alloyce amesema walishirikishwa katika hatua za mradi na wanaahidi kuutunza ili uendelee kuwanufaisha. 
Mwenge wa Uhuru umeendelea kusisitiza ujumbe wa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, ukihimiza wananchi kulinda na kusimamia miradi ya maendeleo kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo. 

Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.”