MRADI WA MAJI KIBIRIKO WAANZA KUTEKELEZWA
Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkoa wa Kihuduma wa Ukonga imeanza kutekeleza Mradi wa Maji uliopo katika eneo la Kibiriko, Mtaa wa Pugu Stesheni, Kata ya Pugu Stesheni, Ilala ambao umelenga kunufaisha wakazi takribani 8,300 katika eneo hilo.
Mradi huo unaolenga kusogeza na kuimarisha huduma ya maji katika eneo hilo la Kibiriko, umeanza utekelezaji kufuatia makabidhiano ya mabomba ya mradi yaliyofanyika Januari 14, 2026 baina ya DAWASA na Viongozi wa Mtaa na Kata ya Pugu Stesheni, mabomba ya maji tayari yameshalazwa kwa umbali wa kilomita 2.25 na utekelezaji wa jumla kufikia asilimia 19.15 hadi sasa.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pugu Stesheni, Ndugu Shukuru Mohamed Mwinjuma amesema baada ya kupokea mabomba ya mradi, ameona jitihada za haraka zinazofanywa na watendaji wa Mamlaka katika kufanikisha mradi huu.
“Mtaa huu awali ulifikiwa na mtandao wa mabomba kwa asilimia 20 tu na kwa ushirikiano wa ofisi ya Mtaa na DAWASA, kufikia tarehe 14 Januari, 2026 tumepokea mradi huu hivyo tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania kwa kutuletea mradi ambao utawafikia wakazi wa Kibiriko kwa asilimia 95.
Tunaona utekelezaji umeanza, binafsi nimeridhishwa na kasi ya mradi inavyoendelea na tunaamini utakamilika kwa wakati," amesema Ndugu Shukuru.
Wakazi wa eneo la Kibiriko, Ndugu Mwamini Abdallah Ngaliwata na Mwajuma Amrani Mussa wamefurahia mradi huo ambao utasaidia kupunguza changamoto zilizopo sasa za upatikanaji wa huduma ya maji katika eneo lao.
“Kwa miaka mingi tumepata shida sana ya maji lakini kwasasa tunashukuru mradi wa maji umepita hapa uwanjani kwangu, tulikuwa tunaenda kuchota maji mabondeni lakini kwasasa tunaona neema imetushukia, tunashukuru kilio chetu kimesikika, tutafaidika na haya maji kwa karibu zaidi,” amesema Ndugu Mwamini.
Kwa upande wake, Ndugu Mwajuma amesema walikuwa wanapata maji mbali visimani na kuna wakati wanakuwa hawana pesa ya kumudu gharama za kununua maji hivyo hukosa huduma hii muhimu, lakini anatarajia mradi huu utakuwa mkombozi wao.
Utekelezaji wa mradi huu mdogo wa maji Kibiriko kwa sasa umefikia asilimia 19.15 na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2026 na kunufaisha Kaya zipatazo 150, hii ni sehemu ya matokeo ya mradi mkubwa wa usambazaji maji Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo) uliotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliokamilika mapema Aprili 2025.
