MRADI WA MAJI KINZUDI–GOBA KUNGURU KUKAMILIKA NOVEMBA
Wakazi 12,814 wa Kinzudi, Goba Kunguru na baadhi ya maeneo ya Goba wanatarajiwa kunufaika na maboresho ya huduma ya maji yatakayolenga kuongeza msukumo wa maji na kuwafikia wananchi ambao bado hawajapata huduma hiyo.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inatekeleza mradi wa kuboresha huduma ya maji kutoka Kinzudi hadi Goba Kunguru, unaohusisha uchimbaji na ulazaji wa mabomba yenye vipenyo vya inchi 12, nane na sita kwa urefu wa kilomita 3.9.
Katika hatua ya maandalizi ya utekelezaji, mabomba yenye kipenyo cha inchi 12 yamekabidhiwa kwa viongozi wa mitaa ya Goba, Goba Kunguru na Kinzudi na Gerald Manongi, aliyemwakilisha Mbunge wa Jimbo la Kibamba, Angela Kairuki.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Manongi ameipongeza DAWASA kwa kuanza kutekeleza ahadi ya kuboresha huduma ya maji katika maeneo hayo na kuiomba Mamlaka kuanza kazi mapema ili wananchi wanufaike kwa wakati.
“Tunaipongeza DAWASA kwa ahadi yenu ya kutuletea mradi wa maji katika eneo hili. Tunaomba, ikiwezekana, mradi huu uanze kutekelezwa kuanzia kesho, Oktoba 29, ili uweze kukamilika mwishoni mwa Novemba, kama mlivyoahidi,” amesema Manongi.
Kwa upande wake, Meneja wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma Ubungo, Mhandisi Anthony Budaga, amesema mradi huo unalenga kuwasaidia wananchi wanaopata maji kwa msukumo mdogo na wale ambao bado hawajafikiwa na huduma hiyo.
“Mradi huu unatekelezwa kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi wanaopata maji kwa msukumo mdogo na wale ambao hawana kabisa huduma ya maji. Tumejipanga kuutekeleza kwa kasi ili wananchi waanze kunufaika na huduma hiyo,” amesema Budaga.
Mradi huo unatarajiwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo husika, kurahisisha shughuli za kila siku na kuboresha maisha ya wakazi zaidi ya 12,800.
Maji yatakayohudumia maeneo hayo yatatoka katika tanki la Salasala, linalopokea maji kutoka Mtambo wa Uzalishaji Maji Ruvu Chini.
DAWASA inatarajia kukamilisha mradi huo mwishoni mwa Novemba 2026.
