Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MRADI WA MAJI MSUMI MKOMBOZI KWA WANANCHI, WABUNGE WAPONGEZI ‎
09 Sep, 2026
MRADI WA MAJI MSUMI MKOMBOZI KWA WANANCHI, WABUNGE WAPONGEZI ‎

Kamati ya Bunge ya Mazingira na Maji, ikiongozwa na Mwenyekiti wake,Mh Jackson Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga imepongeza utekelezaji wa ujenzi wa tanki la maji katika eneo la Msumi, Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, ikisema mradi huo utasaidia kuimarisha upatikanaji wa maji kwa wananchi.
‎
‎Kamati hiyo imetembelea na kukagua maendeleo ya mradi unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), unaohusisha ujenzi wa tanki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 500,000 za maji kwa gharama ya shilingi milioni 996. 
‎
‎Mradi huo unatarajiwa kunufaisha takribani wakazi 22,370 kwa kuongeza uwezo wa kuhifadhi na kusambaza maji katika eneo hilo.
‎
‎Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Mhe. Kiswaga amepongeza kasi ya utekelezaji na kuwataka DAWASA kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa. 
‎
‎Amesema Kamati iko tayari kushirikiana na Serikali na DAWASA katika kutafuta fursa za kuongeza vyanzo vya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi zaidi ya maji Dar es Salaam na Pwani.
‎
‎“DAWASA mnatekeleza dhamira ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji. Mimi pamoja na wajumbe wenzangu tupo tayari kushirikiana nanyi katika kuhakikisha tunaongeza vyanzo vya fedha vitakavyosaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maji,” amesema Mhe. Kiswaga.
‎
‎Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Albert Msando, amepongeza Serikali na DAWASA kwa uwekezaji huo, akisema tanki hilo litakapokamilika litakuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uhakika wa huduma ya maji kwa wakazi wa Msumi.
‎
‎Amesema ziara ya Kamati ni muhimu katika kufuatilia utekelezaji wa mradi hadi ukamilike na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa.