MRADI WA MAJI PANGANI WAANZA

Safari ya kusaka suluhu ya tatizo la maji kwa wananchi zaidi ya 14,868 wa maeneo ya ya Kibaha- Msufini, Lulanzi, TAMCO na Pangani imeanza.
Suluhu hiyo ilianza kusakwa tangu mwaka 2023, uliposainiwa Mradi wa Maji Pangani- Kibaha wenye thamani ya Shilingi bilioni 9.8 mbele ya Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso.
Tayari wahandisi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), wameanza kazi ya kufikisha miundombinu ya ujenzi kwenye eneo la mradi ikiwemo mabomba ya kusafirisha maji ya ukubwa wa inchi 6 yatakayolazwa kwa mita 1,100.
Mradi huo utahusisha kazi ya ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji la ujazo wa milioni 6, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji na ufungaji wa pampu za kusukuma maji pamoja na mita, ujenzi wa bomba kuu la kusafirisha maji la inchi 12 kwa umbali wa kilomita 18.7 pamoja na mabomba ya usambazaji maji ya inchi 8 na inchi 3.
Mradi huu utakuwa na uwezo wa kusafirisha maji kiasi cha lita za ujazo wa milioni 5.2 kwa siku ambayo ni mahitaji ya miaka 20 ijayo.