Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
MRADI WA MAJITAKA MBEZI BEACH UTAKAVYOBORESHA MAZINGIRA
29 Jun, 2026
MRADI WA MAJITAKA MBEZI BEACH UTAKAVYOBORESHA MAZINGIRA

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (DC), Mheshimiwa Saad Mtambule amesema Mradi wa kuboresha Usafi wa Mazingira Mbezi Beach utasaidia kuondoa gharama na changamoto za uondoshaji wa majitaka kwa njia ya kisasa.

Mradi huo unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkandarasi wa Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group na Kampuni ya Metito Overseas kwa gharama ya Shilingi Bilioni 124.

Unahusisha ujenzi wa vituo viwili vya kupokea na kusukuma majitaka, ulazaji na uchimbaji mabomba kwa umbali kilomita 101 pamoja na ujenzi wa chemba 2,383 za kukusanya majitaka. Ukikamilika utanufaisha kaya 4,817 wa Kata ya Wazo, Tegeta, Mbezi Beach, Kunduchi na Kawe.

Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo, Mheshimiwa Mtambule amesema utekelezwaji wa mradi unaenda kwa kasi na unaridhisha kulingana na muda uliopangwa. 

"Nitoe pongezi kwenu kwa kazi kubwa ambayo mnaifanya ya kuhakikisha mradi huu unaenda kukamilika kwa wakati hadi kufika mwezi Oktoba, kazi itakuwa imekamilika," amesema Mheshimiwa Mtambule.

Amesema mradi wa uondoshaji majitaka Mbezi Beach utasaidia kuondoa gharama na changamoto za uondoshaji wa majitaka kwa njia ya kisasa na hivyo kuboresha mazingira.
 
"Mradi huu utaleta matokeo tarajiwa ya kuondoa maji machafu na kwenda kutibiwa ili kusaidia upatikanaji wa nishati safi ya gesi, pamoja na kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuboresha afya za wananchi kwa asilimia kubwa," amesema Mheshimiwa Mtambule.

Amewataka wanufaika wote wa mradi kuwa waangalifu wa miundombinu ya miradi kwa kuepuka kuharibu ili mradi uweze kudumu kwa muda mrefu ulete tija kwa wananchi uweze kutekelezwa kwenye Kata nyingine za Wilaya ya Kinondoni.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mkurugenzi wa Miradi, Mhandisi Christian Christopher amesema mradi huu ni wa kisasa na wa kipekee kutokana na ubora wa kuondosha majitaka majumbani na kuchakata kwenda mtamboni. 

"Utekelezaji unaendelea kwa kasi ili kuhakikisha unakamilika, mpaka sasa kazi ya ujenzi mtambo imefikia asilimia 70 na inatarajiwa mpaka kufika mwezi Oktoba mwaka huu, utakuwa umekwisha kukamilika," amesema Mhandisi Christopher.

Amesema kwa sasa mradi umefikia asilimia 98.6 ambayo ni hatua nzuri zaidi, kwa upande wa maunganisho ya mifumo ya majitaka, jumla ya nyumba 3,600 wa Kata za Kawe, Tegeta, Kunduchi, Wazo na Mbezi Beach wameunganishwa.