MRADI WA USAFI WA MAZINGIRA SINZA C KUBORESHWA AFYA NA MAZINGIRA YA WAKAZI
Takribani kaya 270 za Mtaa wa Sinza C, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, zinatarajiwa kuunganishwa kwenye mtandao rasmi wa uondoshaji majitaka mara baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kukamilisha mradi wa ujenzi wa miundombinu hiyo unaoendelea kutekelezwa katika eneo hilo.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Msimamizi wa Mradi, Mhandisi Gabriel Wanzagi, amesema kazi zinaendelea vizuri na matarajio ni kuukamilisha mwanzoni mwa Septemba 2026.
Ameeleza kuwa mradi huo unahusisha uchimbaji na ulazaji wa mabomba ya majitaka yenye ukubwa wa inchi 10 kwa umbali wa kilomita 4.4 pamoja na ujenzi wa chemba 92 za majitaka.
"Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wote waliokusudiwa wanaunganishwa kwenye mtandao rasmi wa uondoshaji majitaka ili kuzuia uchafuzi wa mazingira unaotokana na utiririshaji wa majitaka kiholela mitaani. Mradi huu utasaidia kuboresha afya za wananchi na mazingira kwa ujumla," amesema Mhandisi Wanzagi.
Ameongeza kuwa eneo la Sinza C halikuwa na mtandao rasmi wa majitaka hapo awali, hivyo kukamilika kwa mradi huo kutatoa suluhisho la kudumu kwa changamoto hiyo. Aidha, amewahimiza wananchi kujiandaa kuunganishiwa huduma hiyo mara itakapokamilika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Sinza C, Fredrick Kapufi, amesema mradi huo utakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha afya za wakazi wa eneo hilo kwa kupunguza hatari ya magonjwa ya mlipuko yanayotokana na uchafuzi wa mazingira.
"Kupatikana kwa huduma hii kutasaidia kuondoa kabisa tabia ya kutiririsha majitaka kiholela na hivyo kulinda afya za wananchi wetu. Huu ni mradi muhimu kwa maendeleo ya jamii yetu," amesema Kapufi.
Naye mkazi wa Sinza C, Ndugu Wales Michael, amepongeza utekelezaji wa mradi huo na kueleza utayari wa wananchi kujiunga na mtandao wa majitaka mara utakapokamilika.
"Tunafurahi kuona suluhisho la kudumu linapatikana. Tunawahamasisha wananchi wote kutumia huduma hii ipasavyo na kuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu hii ili idumu na kuendelea kutunufaisha kwa miaka mingi ijayo," amesema.
Mradi wa uondoshaji majitaka wa Sinza C ni sehemu ya juhudi za DAWASA za kupanua na kuboresha huduma za usafi wa mazingira katika Jiji la Dar es Salaam, kwa lengo la kulinda afya za wananchi, kuimarisha mazingira na kuhakikisha maendeleo endelevu ya miji yanafikiwa.
