MWENGE WA UHURU WAIPA KONGOLE DAWASA UTEKELEZAJI MRADI WA BANGULO

Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, umeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa maji Dar es Salaam ya Kusini maarufu kama "Mradi wa Bangulo" baada ya kuutembelea na kukagua ufanisi wake kwa utakaohudumia Wakazi takribani 450,000 katika majimbo matano ya uchaguzi ya Segerea, Ilala, Ubungo, Temeke na Ukonga.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Ismail Ali Ussi amesema kuwa mradi wa Bangulo umetekelezwa vizuri na kwa kuzingatia viwango vya ubora na kwa umakini mkubwa hivyo kuleta na kuongeza ufanisi kwa wananchi.
Ameongeza kuwa Serikali ya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inahitajika pongezi kwa kufanikisha mradi huu ambao umekuwa Suluhu ya upatikanaji wa maji katika maeneo mengi ya Mkoa wa Dar es Salaam.
"Mwenge wa Uhuru Kitaifa umetembelea na kuridhishwa na umakini wa utekelezaji wa mradi huu na tumejionea namna ulivyozingatia ufanisi, na ubora wa viwango katika utekelezaji wake," amesema Ndugu Ussi.
"Niipongeze DAWASA kwa jitihada kubwa inazofanya za kumsaidia Mhe Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa wananchi wote," amebainisha.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ukonga ambaye pia ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa amesema kuwa mradi huu unaleta furaha kubwa kwa wananchi wa maeneo haya hususani Bangulo ambao kwa muda mrefu hawakuwa na huduma ya uhakika ya kupata maji.
Amesema kuwa kupitia jitihada za Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan leo hii tunashuhudia mradi mkubwa wa Bilioni 36.9 umetekelezwa kwa spidi na kwa ufanisi mkubwa katika eneo hili, kipekee tuna kila sababu ya kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maamuzi haya.
Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema kuwa mradi umehusisha ujenzi wa tenki kubwa la lita milioni 9, ujenzi wa mtandao wa kusambaza maji wa umbali wa kilomita 120, kwa lengo la kunufaisha kaya 450,000 za maeneo tajwa sambamba na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji.
"Kwa sasa mradi umekamilika na tayari zoezi la maunganisho mapya ya maji limeanza ambapo zaidi ya wateja 400 wamejitokeza kuomba huduma ya maji na zaidi ya wateja 200 wamekwisha unganishwa na huduma," amesema Mhandisi Bwire.