Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
NJOMBE WAPONGEZA UWEKEZAJI MIUNDOMBINU DAWASA
27 Jul, 2025
NJOMBE WAPONGEZA UWEKEZAJI MIUNDOMBINU DAWASA

Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Njombe (NJUWASA) imepongeza uwekezaji mkubwa wa Miundombinu ya Uzalishaji na usambazaji Maji uliofanywa na Serikali katika  Mikoa ya Dar es salaam na Pwani iliyosaidia kuimarisha huduma kwa Wananchi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NJUWASA, Ndugu Fidelis Lumato ametoa pongezi hizo wakati wa ziara ya mafunzo ya bodi hiyo katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) ambapo wametembelea mtambo wa uzalishaji maji Ruvu Juu unaozalisha Lita Milioni 196 kwa siku na unaohudumia asilimia 36 ya Wakazi wa Dar es Salaam na Pwani.

"Tumetembea na kujionea uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu ya Maji DAWASA, nipende kuwapongeza kwa kusimamia vyema miundombinu hii inayotegemewa na Wananchi mnaowahudumia" alisema Ndugu Lumato. 

Ndugu Lumato ameongeza kuwa bodi yake imejifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na namna DAWASA inavyopambana na changamoto ya upotevu wa maji na kufurahishwa na mikakati mizuri inayotumika na DAWASA katika kushughulikia changamoto mbalimbali za wateja kwa wakati na kwa Teknolojia za kisasa zaidi na kuahidi kupeleka elimu hiyo NJUWASA

Mhandisi Mkama Bwire, Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, amesema kupitia ujio wa Bodi ya Wakurugenzi NJUWASA wamepata nafasi ya kubadilishana uzoefu wa mambo mbalimbali mtambuka yatakayosaidia kuimarisha huduma kwa Wananchi wanaowahudumia ili kuleta matokeo chanya.