Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
SHILINGI BILIONI 70 ZAWEKEZWA KATIKA MRADI WA MAJITAKA DAR
10 Nov, 2026
SHILINGI BILIONI 70 ZAWEKEZWA KATIKA MRADI WA MAJITAKA DAR

Utekelezaji wa mradi wa uondoshaji na uchakataji wa majitaka wa Buguruni umefikia asilimia 45.3, huku wananchi 181,440 wa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam wakitarajiwa kunufaika na huduma hiyo itakayosaidia kuboresha usafi wa mazingira na kupunguza hatari ya magonjwa yanayohusiana na uchafuzi wa mazingira.

Mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) unalenga kutatua changamoto ya muda mrefu ya uondoshaji majitaka katika eneo la Buguruni, hususan Mtaa wa Mivinjeni, na kupanua huduma hiyo katika maeneo mengine ya Dar es Salaam.

Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, msimamizi wake, Mhandisi Shenyenze Bunyese, amesema kazi ya ujenzi wa miundombinu ya kupokea, kusafirisha na kuchakata majitaka inaendelea katika maeneo mbalimbali ya mradi.

Amesema hadi sasa mabomba yenye kipenyo cha inchi nane yamelazwa kwa urefu wa kilomita 21.9 kati ya kilomita 25.4 zilizopangwa katika kata za Magomeni, Ndugumbi na Mzimuni, sawa na takribani asilimia 86 ya mtandao huo.

Ameeleza kuwa mbali na Buguruni, mradi huo utanufaisha wakazi wa Magomeni, Ndugumbi na Mzimuni katika Manispaa ya Kinondoni, pamoja na Ilala, Mchikichini, Kariakoo, Jangwani, Gerezani, Kisutu, Mchafukoge, Upanga Mashariki, Upanga Magharibi na Kivukoni katika Manispaa ya Ilala.

Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Kolon Global Corporation chini ya usimamizi wa mshauri elekezi, kampuni ya M/s Dohwa Engineering Ltd. Unatarajiwa kukamilika mwaka 2028, baada ya kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu, kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 70.

Mhandisi Bunyese amewataka wananchi kuwa wavumilivu wakati wa utekelezaji wa mradi huo na kushirikiana na DAWASA kulinda miundombinu inayojengwa ili kuhakikisha inakamilika na kutumika kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Makumbusho, Kata ya Mzimuni, Juwi Vumbi, amesema mradi huo unatarajiwa kupunguza changamoto za kiafya zinazoweza kusababishwa na utiririshaji holela wa majitaka na uchafuzi wa mazingira.

Ameipongeza Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya mradi huo, akisema utaimarisha mazingira ya makazi na kunufaisha wananchi wengi.

Naye mkazi wa Mtaa wa Makumbusho, Jumanne Rajab, amesema anaona kazi inayofanyika na kueleza kuwa mradi huo utasaidia kupunguza changamoto ambazo wananchi wamekuwa wakikabiliana nazo kutokana na ukosefu wa mfumo bora wa majitaka.