USOMAJI MITA SHIRIKISHI WAENDELEA KIBAMBA
Watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mkoa wa Kihuduma Kibamba wameendelea na zoezi la usomaji mita kwa kushirikiana na wateja katika maeneo ya Kibamba, Hondogo, Luguruni, Machimbo, Kiluvya ba Mbezi.
Zoezi la usomaji mita linaendelea kutekelezwa na Mamlaka katika kata tano za Wilaya ya Ubungo zenye wateja takribani 53,600 kwa lengo la kuwafikia na kushirikiana nao katika usomaji wa mita za maji pamoja na kuboresha huduma.
Akizungumzia hatua hiyo, Afisa Huduma kwa Wateja DAWASA Kibamba, Juliana Mwendakazi amesema zoezi hilo linaendelea kikamilifu kutokana na ushirikiano unaotolewa na wateja wa kata hizo.
"Tunaendelea na usomaji mita kwa kushirikiana na wateja katika maeneo mbalimbali wamekuwa wakitoa ushirikiano wa hali ya juu kuweza kufanikisha zoezi hili, hivyo tunawasihi zaidi kuendelea kushiriki ili kuepuka changamoto na malalamiko mbalimbali ambayo wanaweza kuhitaji ufafanuzi au elimu zaidi ya usomaji mita," amesema.
Aidha, kupitia zoezi hili linakwenda sambamba na utoaji wa elimu mbalimbali juu ya huduma zinazotolewa na DAWASA ikiwemo uhakiki wa usomaji mita, matumizi sahihi ya maji, njia za malipo na mawasiliano ya Mamlaka pamoja na kutatuliwa changamoto za hapo kwa hapo ikiwa ni njia moja wapo ya uboreshaji zaidi wa huduma.
