SHULE YA MSINGI GOMVU YAFIKIWA NA ELIMU YA HUDUMA ZA MAJI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa elimu katika klabu ya Majisafi na usafi wa Mazingira katika shule ya Msingi Gomvu iliyopo Wilaya ya Kigamboni na kusisitiza juu ya umuhimu wa Maji na Usafi wa Mazingira katika jamii.
Shule hiyo ni miongoni mwa shule 11 za Mazingira zinazosimamiwa na kuendeshwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Afisa Mawasiliano kutoka DAWASA Bi. Hashura Kamugisha ameeleza umuhimu wa Majisafi na usafi wa Mazingira shuleni na maeneo yote yanayotuzunguka, ili kuweka mazingira ya kujifunza safi na salama muda wote.
"Mazingira safi na salama huchochea hali ya kujifinza, mazingira safi ni chachu ya taaluma bora na ni muhimu kwa afya ya akili kwani uepusha magonjwa katika mazingira yetu, hivyo ili kuhakikisha tunaendelea kufurahia mazingira yetu hatuna budi kuyatunza vyema na kujiepusha kutupa taka ovyo na kufuta taratibu zote za usafi zilizopo shuleni" ameeleza Ndugu Kamugisha.
Nae Mwalimu Dorah Deonatus Minga Minzi mlezi wa klabu ya mazingira shuleni hapo ameishukuru Mamlaka kwa jitihada za kutoa elimu ya umuhimu wa maji, pamoja na suala la usafi wa Mazingira kwa wanafunzi.
"Usafi wa Mazingira ni ni muhimu katika jamii hasa kwa maeneo yetu haya ya shuleni kwani hutuepusha na milipuko ya magonjwa mbalimbali yanasababishwa na mazingira machafu,ivo tunawasihi wanafunzi muda wote kuweka mazingira safi yenye kuvutia ufundiahaji na ujifunzaji.Tunawashukuru DAWASA kwa elimu hii ya Usafi wa mazingira." ameeleza Mwl. Dorah.
Kwa upande wake Mwanafunzi Prisca Evaristo, ambae ni mwanachama wa klabu ya maji na usafi wa Mazingira kutoka shuleni hapo, amekiri kufaidika na elimu mbalimbali zinazohusu majisafi na mazingira wanayoipata kila mara kutoka DAWASA.
"DAWASA imekuwa mlezi wa klabu yetu ya mazingira kwa muda sasa na kila mara tunajifunza vitu mbalimbali kuhusu Majisafi na Usafi wa mazingira.Elimu ya leo imesaidia kujenga uelewa zaidi kuhusu utunzaji wa mazingira hasa njia bora na sahihi za kuhifadhi taka ili kuepukana na uchafuzi wa Mazingira.
Mamlaka inasimamia klabu za mazingira shuleni kwa kutoa elimu mbalimbali kuhusu Majisafi na Usafi wa mazingira, utunzaji wa miundombinu ya maji,utunzaji wa vyanzo vya maji na kuwaandaa wanafunzi katika rika lao kuwa mabalozi wema katika jamii katika masuala yote yanayohusu maji.
