SIKU 14 ZATENGWA KUWATAMBUA WATOA HUDUMA MAGARI YA MAJITAKA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetenga siku 14 kuanzia tarehe 26.1.2026 hadi tarehe 8.2.2026 za utoaji wa vibali kwa watoa huduma ya uondoshaji majitaka kupitia magari Jijini Dar es Salaam.
Zoezi hili la kawaida la utambuzi, usajili na utoaji wa vibali linatarajia kufanyika katika mabwawa ya kuchakata Majitaka ya Kurasini, likiwa na lengo la kuratibu huduma ya majitaka kupitia magari kwa kuhakikisha majitaka yanayotolewa katika maeneo mbalimbali yanapelekwa kwenye mabwawa ya kutibu na kuchakata majitaka yanayosimamiwa na DAWASA na sio vingenevyo.
Katika zoezi hili, Wamiliki na waendeshaji wanaombwa kufika na nyaraka mbalimbali ikiwemo kopi ya kadi ya usajili wa gari, kopi ya fomu/cheti cha ukaguzi wa uzito na vipimo, kopi ya leseni ya dereva anayeendesha chombo husika, kopi ya kitambulisho cha NIDA ya mmiliki wa gari na namba ya leseni ya biashara (TIN number)
Mkurugenzi wa huduma za Usafi wa Mazingira DAWASA, Mhandisi Lydia Ndibalema amesema baada ya muda wa usajili kupita, mtoa huduma kutoa huduma za majitaka bila kibali hai cha uendeshaji atachukuliwa hatua za kisheria.
"Magari yote yatakayopata vibali vya uendeshaji yatabandikwa stika maalumu za DAWASA, na Taasisi/Kampuni zinazomiliki magari binafsi ya majitaka zinatakiwa kushiriki zoezi hili," amesena Mhandisi Mwanjee.
Mwenendo wa usajili na utoaji wa vibali vya uendeshaji wa magari ya Majitaka yanayotoa huduma katika eneo la DAWASA ni jumla ya vibali 622 kuanzia 2020 hadi 2024
