SULUHU YA MAJISAFI YAPATIKANA MAKANGARAWE
Changamoto ya upatikanaji wa majisafi kwa wananchi wa mtaa na kata ya Makangarawe, Wilaya ya Temeke imepatiwa suluhu kwa kuchimbwa kisima cha majisafi huku wakitakiwa kulinda miundombinu yake.
Mradi wa kisima hicho chenye urefu wa mita 120, ujenzi na uwekaji tenki la maji la lita 10,000 pamoja na ulazaji mabomba ya usambazaji maji kwa wananchi, unatekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Msimamizi wa Mradi huo, Mhandisi Baraka Masoro amesema mradi wa kisima cha maji unatarajia kukamilika Aprili 10, 2026 na unakusudia kuboresha hali ya upatikanaji wa maji katika Mtaa wa Makangarawe hivyo amewasihi wananchi kulinda miundombinu ya maji katika mradi huu muhimu.
"Utekelezaji wa mradi huu unaendelea, wakazi wa Mtaa wa Makangarawe watapata maji safi na salama siku chache zijazo hivyo tunawasihi wananchi kulinda na kutunza miundombinu ya mradi ili huduma iwe endelevu,” amesema Mhandisi Masoro.
Aidha amewaomba wanapoona tatizo lolote kuhusu maji watoe taarifa DAWASA kwa kupiga simu huduma kwa wateja namba 181 bila ya malipo na tutafanyia kazi kwa wakati.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Makangarawe, Ndugu Mhina Ramadhani Mfikirwa, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania kupitia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia mradi huu wa maji wa kihistoria katika Mtaa huo.
"Tunaishukuru Serikali na timu yote ya DAWASA kwa kuleta mradi huu wa majisafi ambao unatuletea matumaini na hamasa kwani tangu mwaka 1961 wananchi wa Makangarawe hawajapata maji ya DAWASA moja kwa moja hivyo kuja kwa huu mradi tumefurahi.
Tulikuwa tunatumia visima vya watu binafsi kupata maji kwa gharama kubwa sana, lakini sasa kwa huu mradi wananchi wamekomboka na adha ya maji," amesema Ndugu Mfikirwa.
Naye Mkazi wa Makangarawe, Ndugu Mwajuma Ramadhani ameeleza mradi huu wa maji utawapunguzia kero ya kutumia muda na gharama kubwa ya fedha kwa ajili ya maji.
"Tunafuraha sana sisi wamama kwa serikali kutuletea mradi huu mtaani kwetu, maji tunapata mbali kwa bei kubwa kati ya Shilingi 700 hadi 1,000 kwa ujazo wa lita 20 na hatuna uhakika na usalama wa maji hayo. Kwa sasa itatupunguzia changamoto za maji na7 kupunguza gharama za matumizi ya nyumbani," amesema Ndugu Mwajuma.
